LUGOLA AUNDA KAMATI YA KUCHUNGA MALALAMIKO YA RUSHWA KWA POLISI WA USALAMA BARABARANI

Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola amemuagiza katibu mkuu wa wizara hiyo aunde kamati ya kuchunguza vitendo na mianya ya rushwa kwa jeshi la polisi na msisitizo mkubwa kwenye kitengo cha usalama wa barabarani.

Akizungumza leo Jumatano Januari 16 2019, Lugola pia amemtaka kamanda wa kikosi cha usalama wa barabarani kujitafakari, kujipima kama anatosha katika nafasi hiyo.


"Nimemwelekeza katibu mkuu aunde timu ambayo itapewa miezi mitatu kuchunguza vitendo na mianya ya rushwa na msisitizo mkubwa kwenye usalama wa barabarani na tume hiyo itanipa hatua za kuchukua," amesema.


Amesema kumekuwa na malalamiko mengi yanayohusu ubambikiaji wa makosa ya barabarani kwa madhumuni ya kutaka rushwa na unyanyasaji wa madereva bodaboda.


Ameongeza kwamba licha ya kuwapo makamanda wa trafiki wa mikoa lakini bado kumekuwa na malalamiko juu ya utendaji wa polisi na hivyo ameamua kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo.


Amesema tume itachunguza kitengo hicho na kumpelekea majibu ili aweze kuchukua hatua.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527