CCM YAUNGA MKONO SHERIA MPYA YA VYAMA VYA SIASA

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, amesema sheria vya vyama vya siasa iliyopo sasa haimpi nguvu Msajili wa Vyama vya Siasa kufanya kazi kwa ufanisi hivyo mabadiliko ya muswada mpya yatasaidia uimara wa vyama vya siasa na Ofisi ya Msajili kufanya kazi kwa ufanisi.

Polepole ameyasema hayo leo Jumatano Januari 16 katika mkutano wa chama hicho wa kujadili mabadiliko ya muswada kabla ya kupelekwa Bungeni uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

“Mabadiliko hayo yatampa nguvu msajili wa vyama vya siasa kutazama kwa jicho la upole endapo chama kimefanya vizuri na jicho la ukali kwa mambo ya ovyo ambayo chama kitafanya,” amesema.

Aidha, amesema mabadiliko hayo yatampa nguvu Msajili kuhusika kwenye usajili wa vyama vya siasa, kusimamia chaguzi za vyama vya ndani, kutoa na kufuatilia uwajibikaji wa ruzuku.

“Sheria tunayoitumia sasa ni sheria ya mwaka 2010 ni miaka 10 imepita tangu kufanya mabadiliko ya sheria, sisi ni vijana tunatakiwa tutoe maoni na mabadiliko ya sheria mpya ili sheria mpya itakayokuja kutumika isiweze kumbana msajili wa vyama vya siasa pamoja na sisi wanachama,” amesema Polepole.


Awali katibu wa siasa na mahusiano ya kimataifa wa CCM, Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga amewataka wanachana wa chama hicho kutoa maoni yao bila wasiwasi kuhusu muswada huo.

Amesema kusudi kubwa la muswada huo ni kutengeneza mazingira ya kuwaongoza Watanzania kulingana na mazingira yaliyopo.

Amesema muswada huo unapiga marufuku kuanzishwa kwa vikundi vya ulinzi na usalama ndani ya vyama vya siasa jambo ambalo ni sahihi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post