KATIBU WA CCM WILAYA AKAMATWA KWENYE MAANDAMANO

Katibu wa CCM wilaya ya Hai, Laurence Kumotola, amekamatwa na polisi kwa tuhuma ya kuwazuia askari kufanya kazi yao ya ulinzi, wakati wakitaka kuingia katika ofisi za halmashauri ya wilaya ya Hai.

Tukio hilo limetokea leo majira ya saa 5:45 asubuhi, wakati katibu huyo akiwa ameambatana na wafuasi wa chama hicho pamoja na viongozi mbalimbali, walipodaiwa kuvamia ofisi ya mkuu wa wilaya kwa maandamano na kuzuia watu kuingia katika ofisi hizo hadi wao watakaporuhusiwa na kusikilizwa na mkuu wa wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya.

Katibu huyo akiwa na wafuasi hao, walitumia zaidi ya dakika 10 wakiwa katika geti la kuingia katika ofisi hizo, hadi pale mkuu wa wilaya ya Hai alipotoka na kuruhusu wafunguliwe awasikilize.

Wakati mkuu huyo wa wilaya akizungumza na watu hao, ndipo mkuu wa polisi wilaya ya Hai, Lwelwe Mpina alipoingia na kumwambia mkuu wa wilaya kuwa anamkamata katibu wa CCM kwa kuwa amemzuia kufanya kazi yake.

"Mkuu naomba kumchukua katibu, amenizuia kuingia hapa wakati mimi ndiye nasimamia ulinzi na usalama hapa," alisema OCD.

Akizungumza na waandamanaji hao, Lengai Ole Sabaya amesema hakuna kiongozi yeyote atakayeruhusiwa kulizuia jeshi kufanya kazi na yeyote atakayefanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.

"Tumesitisha ufanyaji wa siasa kwa vyama vyote kwa sababu uchaguzi bado haujafika na hata tulipofikia kwa sasa mtu yeyote atakayehusika kulizuia jeshi la polisi achukuliwe hatua."

"Na nyinyi CCM kama mnalalamika mtumie njia ambayo ni rasmi lakini si kufanya maandamano." ameongeza Sabaya

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post