DIWANI WA CCM AVAMIWA KWA SHOKA NA NONDO KAHAMA


Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao

Diwani wa kata ya Sabasabini halmashauri ya wilaya ya Ushetu wilayani Kahama Emmanuel Makashi (49) kupitia Chama Cha Mapinduzi amenusurika kifo baada ya watu wasiofahamika kuvunja nyumba yake kwa shoka na nondo na kumjeruhi kichwani na mkononi na kufanikiwa kupora shilingi milioni 5.


Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao tukio hilo limetokea Januari 3,2019 majira ya saa saba kamili usiku katika kijiji cha Ifunde, kata ya Mpunze, tarafa ya Dakama, wilaya ya Kipolisi Ushetu na mkoa wa Shinyanga.

Kamanda Abwao amesema watu watatu wasiofahamika walivunja nyumba ya Emmanuel Makashi diwani wa kata ya Sabasabini kwa kutumia shoka na nondo kisha kuiba pesa zinazokadiriwa kuwa ni Tshs 5,000,000/=.

"Katika kupambana na wahalifu hao,diwani huyo alipata michubuko kichwani na mikononi na kutibiwa katika hospitali ya Halmashauri Mji wa Kahama na hali yake inaendelea vizuri",ameeleza. 

Amesema chanzo cha tukio hilo ni kuwania mali.

“Aidha, mmoja kati ya wahalifu hao aitwaye Yohana Masanja (19) mkazi wa kijiji cha Lowa alikamatwa na kuuawa kwa kuchomwa moto na wananchi waliojichukulia sheria mkononi, Juhudi za kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa wengine waliohusika na tukio zinaendelea”,amesema  Kamanda Abwao.

Na Kadama Malunde – Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527