DIAMOND PLATNUMZ, RAYVANNY WAFUNGIWA KUFANYA SANAA.....TAMASHA LA WASAFI FESTIVAL LAFUTWA


Diamond Platnumz na Rayvanny wamefungiwa kufanya onyesho lolote ndani na nje ya Tanzania na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Baraza hilo limesema marufuku hiyo ya muda usiojulikana inaanza kutekelezwa leo.

Wasanii hao wawili walikuwa awali wametakiwa kuuondoa wimbo wao kwa jina 'Mwanza' kutoka kwenye mitandao ya kijamii, lakini wimbo huo umeendelea kuwepo kwenye YouTube.

Aidha, wameendelea kuucheza kwenye matamasha.

"Baraza limefikia maamuzi ya kuwafungia rasmi kutokana na wasanii hawa kuendelea kuonyesha dharau na utovu wa nidhamu kwa mamlaka zinazosimamia masuala ya sanaa nchini na uvunjifu wa maadili uliokithiri unaofanywa na waandaaji wa Tamasha la Wasafi 2018, chini ya uongozi wake Diamond Platnumz," taarifa ya Basata ambayo imetiwa saini na Onesmo Kayanda kwa niaba ya Katibu Mtendaji inasema.

"Pamoja na maelezo hayo, Baraza linatoa taarifa kuwa kibali cha Tamasha la Wasafi 2018 kimesitishwa kutokana na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu katika uendeshaji wa tamasha hilo hapa nchini."

Basata walitangaza kuufungia wimbo wa Mwanza mnamo 12 Novemba kwa kile walichosema ni "kwa kubeba maudhui machafu."

"Lebo ya Wasafi, wasanii wake sambamba na vyombo vya habari vinapewa onyo na tahadhari kuendelea kutumia wimbo huu kwa namna yoyote ile," baraza hilo lilisema.

Baraza hilo lilisema wimbo huo una "ukiukwaji mkubwa wa maadili ya Kitanzania" na kwamba umetumia "maneno yanayohamasisha ngono.

Baraza hilo wakati huo liliwaonga wasanii waliohusika, Rayvanny na Diamond, pamoja na uongozi wa Wasafi Limited kufuata sheria na "kutoutumia wimbo huo na nyimbo nyingine zilizofungiwa kwa namna yoyote ile."

Baraza hilo liliwataka "kuuondoa wimbo huo mara moja kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kufika saa kumi kamili" siku hiyo.

Taarifa hiyo ilitiwa saini na Katibu Mtendaji wa Basata Godfrey Mngereza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527