WANAOFANYA BIASHARA MTANDAONI SASA KULIPA KODI

Wafanyabiashara wanaofanya biashara kupitia mitandao mbalimbali wametakiwa kufika katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili wajiandikishe waanze kulipa kodi kwa mujibu wa sheria kama wafanyabiashara wengine wote.

Hayo yamesemwa na Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere jana asubuhi alipokuwa akizungumza kupitia Clouds FM kuhusu mbinu mbalimbali wanazokusudia kuzitumia ili kuhakikisha kuwa wanaongeza idadi ya walipa kodi na kuongeza mapato.

Kamishna Kichere alilazimika kutoa maelezo hayo baada ya kuhojiwa na mtangazaji kuhusu uwepo wa watanzania wachache wanaolipa kodi (zaidi ya milioni 2) wakati jumla ya Watanzania wapo takribani milioni 55.

Akizungumzia mkakati wa TRA kuongeza idadi ya walipakodi, kamishna huyo alisema wameanza kuwafikia watu wanaofanya biashara mitandaoni ambao wamekidhi vigezo vya kutakiwa kulipa kodi, wawe wanalipa kodi kama wafanyabiashara wengine.

Alieleza kuwa, wafanyabishara ambao thamani ya biashara zao ni zaidi ya shilingi milioni nne wanatakiwa kufika TRA wajiandikishe ili wapate Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi (TIN) waanze kulipa kodi.

“Wapo watu wanafanya biashara za bidhaa mbalimbali kwa njia ya mtandao na wanapata wateja ambao huwasambazia bidhaa husika, sasa tunawataka walipe kodi kama wengine,” Kayombo alisema.

“Hizo ni biashara za kawaida kama nyingine zinafanyika kwa njia ya mtandaoni tu.”

Alisema wafanyabiashara hao ni kama wa 'Uber' (magari yanayobeba abiria walioyaita kwa njia ya mtandao) ambao awali walikuwa hawalipi kodi lakini kwa sasa wanalipa na ni biashara ambayo inafanyika mtandaoni.

Alipoulizwa juu ya namna ya kuwadhibiti na kuwapata walipakodi hao, Kayombo alisema TRA itawafuatilia kwenye mitandao wanapotangazia biashara zao na kuwataka walipe kodi kwa mujibu wa sheria kabla ya kufuatwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post