BIDHAA ZENYE KILEVI KUTOZWA USHURU KIELEKTRONIKI


Bidhaa zinazostahili kutozwa ushuru wa bidhaa kama vile sigara, mvinyo, pombe kali pamoja na bia zitaanza kutumia rasmi stempu za kielektroniki Januari, 2019 katika Mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Shinyanga na Mbeya ambapo mfumo wa stempu hizo umeshafungwa kwenye mitambo ya uzalishaji.
Akizungumza mara baada ya kumaliza kukagua ufungaji wa mfumo huo katika Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) na Kiwanda cha kutengeneza vinywaji vikali cha Nyati Spirit Tanzania jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere alisema kuwa mfumo huo mpya unaondoa mfumo wa zamani wa stempu za karatasi.

“Nimekuja kufanya ziara katika viwanda hivi ili kujiridhisha kama kweli mfumo huu wa stepu za kielektroniki umefungwa na nimejionea mwenyewe mfumo tayari umefungwa katika viwanda vyote nilivyotembelea. Hivyo, tunaachana na mfumo wa zamani wa stempu za karatasi na kwa sasa tunaendelea kufunga mfumo huu mpya wa stempu za kielektroniki kwenye mikoa mingine ambayo haitaanza katika awamu hii”, alisema Kichere.

Kichere alisema kuwa lengo la kuweka stempu za kielektroniki kwenye bidhaa hizo ni kupata idadi halisi ya uzalishaji wa bidhaa ili kutoza kodi stahiki na kuondoa dhana ya kusema kwamba TRA inawaonea wafanyabiashara wanaozalisha bidhaa hizo kwa kutoza kodi isiyoendana na uzalishaji.

“Lengo la kuweka stempu hizi za kielektroniki ni kupata kiasi halisi cha uzalishaji wa bidhaa hizi ili kila upande uridhike yaani mzalishaji alipe kodi sahihi na sisi TRA tutoze kodi stahiki bila kupingana wala kugombana na wateja wetu”, alisema Kichere.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda cha kutengeneza vinywaji vikali cha Nyati Spirit Tanzania Rupa Suchak amesema kuwa amefurahishwa na kitendo cha serikali kufunga mfumo huo wa stempu za kielektroniki kwa sababu serikali itaongeza mapato na wafanyabiashara wataongeza uhiari wa kulipa kodi.

“Ninaishukuru sana serikali yetu kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kuleta mfumo huu mpya ambao utaongeza mapato na kupanua wigo wa kodi lakini pia kwetu sisi wafanyabiashara tutaongeza uhiari wa kulipa kodi”, alisema Rupa.

Uwekwaji wa stempu za kielektroniki katika bidhaa nyingine kama vile juisi, maji ya chupa, bidhaa za muziki na filamu (CD\DVD\Tape) zitafuata kwa tarehe ambayo itatangazwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania hapo badae.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post