ISANGULA : WENYE MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI SIYO WATENDA DHAMBI...ELIMU INATAKIWA

Mshauri Nasaha kutoka Hospitali ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza,Yahaya Isangula.

Jamii imetakiwa kuachana na mitazamo hasi kuhusu Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa kuamini kuwa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU ni watenda dhambi.

Kauli hiyo imetolewa na Mshauri Nasaha kutoka Hospitali ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Bw. Yahaya Isangula alipokuwa akiwasilisha mada ya 'Unyanyapaa' katika Kambi ya Watoto na Vijana ya Ariel 2018 inayoendelea katika hoteli ya Serene, jijini Dar es salaam.

Bw. Isangula alisema bado jamii haina elimu ya kutosha kuhusu VVU na UKIMWI hivyo kuwaomba wadau kuendelea kushirikiana na serikali kufikisha elimu kwa jamii ili kuepuka vitendo vya kunyanyapaa na kuwatenga watu wenye maambukizi ya VVU.

Alisema uelewa duni kuhusu VVU na UKIMWI unasababisha kuwepo kwa unyanyapaa hivyo kupelekea watu wanaoishi na maambukizi ya VVU kushindwa kupata msaada wa kijamii na kimatibabu. 

“Bado kuna wanaoamini kuwa mtu mwenye maambukizi ya VVU ni mtenda dhambi,wanasema waliopata VVU walitenda dhambi ya kufanya ngono,watu hawa wanafikiri VVU vinapatikana kwa kufanya ngono tu,hawajui kuwa maambukizi yanatokea kwa njia nyingi,” alieleza. 

Alizitaja njia zinazosababisha maambukizi ya VVU kuwa ni pamoja na kuchangia vitu vyenye ncha kali, kuongezewa damu yenye maambukizi ya VVU, maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito kujifungua na kunyonyesha lakini pia kufanya ngono zembe.

Kambi hiyo ya Ariel 2018 iliyoanza Disemba 10,2018 imeshirikisha watoto na vijana 50 kutoka mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mara na Mwanza ambao pia ni wanachama wa klabu zinazosimamiwa na asasi ya Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) inayolenga kutokomeza VVU na UKIMWI kwa watoto na familia.

Kwa upande wake, Bi. Mwanaharusi Mohamed, aliwataka watu wanaoishi na maambukizi ya VVU kutokata tamaa kwani kuwa na maambukizi ya VVU siyo mwisho wa maisha.


Mwanaharusi Mohamed akieleza kwamba pamoja na kupata kwake maambukizi ya VVU wakati wa kuzaliwa ni mwenye afya njema na anaamini kuwa ndoto zake hazitakwamishwa na maambukizi.
Mshauri Nasaha kutoka Hospitali ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Bw. Yahaya Isangula, akizungumza kwenye Kambi ya Ariel 2018 katika hoteli ya Serene, jijini Dar es salaam leo Jumatano Disemba 22,2018.
Bw. Isangula akiendelea na mada ukumbini.
Vijana na watoto wakicheza ukumbini.
Mwalimu Lugano Maclean wa taasisi ya Babawatoto akizungumza na watoto na vijana wakati wa Ariel Camp. 
Watoto wakichora michoro mbalimbali wakati wa Ariel Camp.
Watoto wakiwa katika pozi.

Mwalimu Lugano Maclean kutoka taasisi ya Babawatoto akitoa mada kwenye Kambi ya Ariel 2018

Vijana wakielezea maisha yao kwa kuchora

Watoto wakiendelea kuelezea maisha yao kwa sanaa ya kuchora.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527