UCSAF WAWEZESHA UZINDUZI WA MNARA WA VODACOM USHETU KAHAMA


Muonekano wa Mnara unaomilikiwa na kampuni ya Vodacom uliozinduliwa katika halmashauri ya wilaya ya Ushetu.


Zaidi ya wananchi 50,000 kutoka kata tano za Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambao walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya mawasiliano kwa muda mrefu,hatimaye wamepata huduma hiyo kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF).

Wakizungumza jana katika hafla ya uzinduzi wa mnara unaomilikiwa na kampuni ya Vodacom ambao umejengwa na serikali kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote,wananchi hao walisema walikuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma ya mawasiliano kwa baadhi ya kata ambazo mtandao unakamata/unapatikana.

Mmoja wa wananchi hao Elias Zakaria mkazi wa kata ya Nyamilangano alisema walikuwa wakitembea umbali wa zaidi ya kilomita 100 kufika Kahama Mjini kutafuta huduma ya mawasiliano hali ambayo ilikuwa ikikwamisha shughuli za maendeleo katika maeneo yao.

Ofisa Mjendaji wa kijiji cha Nyamilangano Namana Shabani alisema walikuwa wanapata shida ya mawasiliano katika kuwaalika wajumbe wa serikali ya kijiji katika mikutano ya maendeleo ambapo njia iliyokuwa ikitumika ni barua au kuwafuata wajumbe nyumbani kwao.

“Tulikuwa tunapata shida kuwaalika wajumbe wa serikali ya kijiji na kata kuhudhuria kikao cha maendeleoa, na mfumo ambao tulikuwa tunautumia kuwapa taarifa ilikuwa ni kuwatumia barua ama kuwafuata nyumbani mjumbe mmoja baada ya mwingine hali ambayo ilikuwa inakwamisha shughuli za maendeleo kwenda kwa wakati”,alisema Shabani.

Hata hivyo, Katibu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote nchini (UCSAF) Justina Mashiba alisema mpaka sasa zaidi ya Minara 530 imeshafungwa katika kata mbalimbali nchi nzima na zaidi ya wananchi milioni nne wameshanufaika na huduma ya mawasiliano kwa wote vijijini.

Alisema mnamo tarehe 13 mwezi Disemba mwaka huu wameshasaini mikataba na makampuni ya simu kwa ajili ya ujenzi wa minara 173 katika maeneo ambayo yana changamoto ya mawasiliano nchini.

Naye mwenyekiti wa Mfuko huo Joseph Kilongola alisema wamekuwa walikijenga minara katika kata zenye mvuto wa kibiashara na kuongeza kuwa ifikapo mwaka 2020 kila sehemu zenye changamoto ya mawasiliano nchini zitakuwa zimepata huduma hiyo.

Kwa upande wake Meneja wa Kampuni ya Vodacom wilaya ya Kahama, Jovity Ikate alisema Halmashauri ya Ushetu ina jumla ya minara 10 kati hiyo minara miwili imejengwa na Serikali kwa asilimia 100 na kuwataka wananchi wa kata hizo kuchangamkia fursa za kibiashara kupitia huduma ya mawasiliano.

Naibu Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ushetu Elias Kwandikwa alisema kupatikana kwa mnara huo kutasaidia kupunguza adha kwa wananchi na watumishi wa Halmashauri hiyo kusafiri umbali mrefu kufua huduma ya mawasiliano.

Aliongeza kuwa serikali kupitia mfuko huo itaendelea kutoa huduma ya mawasiliano katika maeneo yote ambayo yana changamoto ya huduma ya mawasiliano ili kuongeza chachu ya maendeleo katika kata na vijiji.

Na Salvatory Ntandu - Kahama

Naibu waziri wa Ujenzi Elias Kwandikwa akikata utepe ikiwa ni ishara ya kuuzindua mnara wa Vodacom katika kijiji cha Nyamilangano Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga.
Meneja wa Vodacom wilaya ya Kahama Jovin Ikate akisoma taarifa ya ujenzi wa Mnara huo katika hafla ya uzinduzi wa Mnara huo katika kijiji cha Nyamilangano.
Katibu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote nchini (UCSAF) akizungumza na Wananchi na viongozi waliohudhuria Hafla ya uzindunzi wa mnara wa Vodacom ambao umejengwa kwan ufadhili wa serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527