MNYIKA AMPONGEZA RAIS MAGUFULI, AMUOMBA AFANYE UBINADAMU... MWENYEWE AGOMA

Mbunge wa Jimbo la Kibamba kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), John Mnyika amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa kuweza kuamua kujenga barabara ya njia nane.

Amesema kuwa Watanzania wamemuombea asiwe na kiburi, huku akisema Wananchi wana malalamiko juu ya Bomoabomoa ambapo amemuomba kutanguliza utu, wa Mwl. Nyerere mbele.

Aidha, Mnyika ameongeza kuwa maendeleo ni ya vitu lakini maendeleo zaidi ni ya watu huku akimtaka atafakari kuwalipia fidia Wananchi waliopisha ujenzi huu.

“Kuna hili suala la bomoabomoa tunaomba ubinadamu utumike kwa kuwalipa fidia wananchi ili kuondoa malalamiko yaliyopo,” amesema.

Mbali na suala hilo la bomoabomoa, Mnyika pia amemuomba Rais Magufuli kuondoa vikwazo vinavyoikabili demokrasia nchini.

”Demokrasia na Maendeleo ni mapacha, tunakuomba Rais unapofanya kazi za Miradi ya Maendeleo vilevile ukatumia fursa hii kuzungumzia kuondoa vikwazo vinavyoikabili Demokrasia ya Nchi ambayo tunaamini vitasaidia Nchi kusonga mbele,”amesema Mnyika.

Pia ameongeza kuwa kuna mambo matano yanatoka kwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambayo anawaomba Watanzania na Rais kwa ujumla kuweza kuyatafakari kwa muda huu tunapoelekea mwaka 2019.

Mnyika amesema kuwa akisikia Wafanyakazi wa Umma wanalilia kikokotoo, wengine wamepandishwa madaraja hawajapandishwa mishahara, Wafanyabiashara wanalia Mtaani, na kumuomba akipata nafasi ya kuzungumza pamoja na uzinduzi utatoa matumaini ya Taifa kwa 2019 na 2020″.

Hata hivyo,Rais John Magufuli amemgomea John Mnyika, Mbunge wa Kibamba na Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo kuhusu ombi lao la kuitaka serikali kuwalipa fidia wakazi wa Kimara na Mbezi waliobomolewa nyumba ili kupisha mradi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha. 

 Rais Magufuli amesisitiza kwamba serikali haitalipa fidia kwa watu waliobomolewa nyumba zao kupisha upanuzi wa barabara hiyo, kwa kuwa walijenga ndani ya hifadhi ya barabara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post