MCHINA AKAMATWA NA MADINI YA TANZANITE



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Kamishna Msaidizi wa Polisi, Hamis Issa amethibitisha kukamatwa kwa madini ghafi mbalimbali ikiwemo madini yanayopatikana Tanzania pekee aina ya Tanzanite ambayo yalikuwa yamebebwa na raia wa kigeni mwenye asili ya China kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Kamanda Hamis Issa amesema tukio la kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo limetokea kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Kilimanjaro, ambapo madini mengine aliyokutwa nayo ni aina ya Salfa, Ruby, Safaya na Almadite.

Aidha amesema kuwa zoezi hilo limefanikiwa kwa msaada wa mashine za kisasa za kukagulia mizigo na abiria zilizofungwa katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA), kupitia Kitengo cha Usalama cha kiwanja hicho ambapo madini hayo yalikuwa na uzito wa gramu 1118.

Ameongeza kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 22 mwaka huu, ambapo wakiwa katika ukaguzi wa mizigo ya abiria askari maalumu kitengo cha ukaguzi na usalama walifanikiwa kubaini mzigo wa madini hayo ambao ulikuwa umefungwa kwa umahiri wa hali ya juu ili isiwe rahisi kutambulika.

Imeelezwa kuwa madini hayo yana thamani ya zaidi ya shilingi milioni 40 za kitanzania ambapo mtuhumiwa ametozwa faini ya shilingi milioni nne kama adhabu.
Chanzo - Eatv

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post