KAMERA ZAMUUMBUA SHABIKI UWANJANI ALIYEMPIGA CHUPA YA KICHWA MCHEZAJI


Mashabiki katika uwanja wa Emirates

Klabu ya soka ya Arsenal imethibitisha kuwa kwa msaada wa kamera za usalama 'CCTV Camera' katika uwanja wa Emirates, wamefanikiwa kumbaini shabiki ambaye alimpiga na chupa ya maji kichwani mchezaji Dele Alli wa klabu ya Tottenham.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya Habari, Arsenal imesema picha zimeonesha shabiki huyo akiwa anarusha chupa ya maji kisha akaondoka uwanjani baada ya tukio hilo.

Tukio hilo ambalo lilitokea kwenye mchezo wa robo fainali ya kombe la Carabao ama EFL, ambapo shabiki alirusha Chupa ya maji iliompiga kichwani kiungo huyo wa Tottenham na timu ya taifa ya England wakati alipokuwa akiufuata mpira uliotoka nje ya uwanja.


Dele Alli mwenye jezi namba 20 alipopigwa na chupa kichwani.

''Klabu inalaani kitendo hiki kwani Emirates sio mahala pa matukio ya aina hiyo na tayari tumeshapata picha za mtu huyo, polisi wa Metropolitan jijini London wanaendelea kumsaka shabiki huyo'', imeeleza taarifa ya Arsenal.

Katika mchezo huo ilishuhudia Arsenal ikifungwa mabao 2-0 nyumbani hivyo kutupwa nje katika mashindano hayo. Mabao ya Tottenham yalifungwa na Dele Alli aliyefunga bao la pili huku lile la kwanza likifungwa na Heung-Min Son, ambapo sasa itakutana na Chelsea katika hatua ya nusu fainali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post