Picha : BODABODA KISHAPU WAANZISHA MRADI WA SAMAKI....RTO AWATAKA WASITUMIE FAIDA KULIPA FAINI


Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga (RTO) Anthony Gwandu, amezindua mradi wa ufugaji samaki kwa kikundi cha waendesha bodaboda wilayani Kishapu, kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.


Uzinduzi huo umefanyika jana Desemba 15, 2018 jirani na Mto Tungu mahali ambapo lilipo bwawa hilo la ufugaji samaki, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na maofisa wa Polisi wa kikosi cha usalama barabarani wilaya na mkoa.

Akizungumzia mradi huo, mwenyekiti wa kikundi cha Bodaboda wilayani Kishapu Daniel Eva, alisema walipata wazo hilo baada ya kuona maisha ni magumu, na hivyo kuamua kuanzisha mradi huo wa ufugaji Samaki aina ya Kambale, ambao watakuwa wakiwauza ili kujipatia fedha kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Alisema kikundi chao kina jumla ya wanachama 50 ambapo walichangisha fedha na kufikisha Shilingi Milioni mbili, ndipo wakatafuta mtaalamu wa kuwapatia elimu hiyo ya ufugaji Samaki kutoka Shirika la REDESO kwa kushirikiana na maofisa uvuvi.

“Kwenye kikundi chetu cha bodaboda huwa tunakopeshana fedha na kurudisha kwa riba, ndipo tukaona ni bora kuanzisha miradi ambayo itatusaidia kujikwamua kiuchumi na tumeanza na mradi huu wa ufugaji Samaki aina ya Kambale,”alisema Eva.

Naye mwenyekiti wa mradi huo wa ufugaji Samaki Salumu Geogre, alisema vichanga vya Samaki hao Kambale 2,000 walivifuata jijini Mwanza kwa kununua kila kimoja Shilingi 200 ambapo ndani ya miezi Sita wanatarajia kuvuna na kuuza kwa Shilingi 5,000 hadi 6,000.

Kwa upande wake mkuu wa kikosi cha usalama barabarani Mkoani Shinyanga Anthony Gwandu, aliwapongeza bodaboda hao kwa kuanzisha mradi wa kujikwamua kiuchumi na kutoa wito kwao watii sheria za usalama barabarani, ili fedha watakazozipata kwenye mradi huo wazitumie kwenye maendeleo na siyo kuishia kulipa faini.

Alisema jambo waliloanzisha kikundi hicho cha bodaboda wilayani Kishapu, kinapaswa kuigwa na vikundi vingine na kuondoa dhana ya kudharaulika, ili kazi hiyo ipate kuheshimiwa na kuonekana kama ajira nyingine, pamoja na kuacha kujiingiza kwenye masuala ya kihalifu ili mkoa ubaki salama na tulivu kama ulivyo sasa.

TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga Anthony Gwandu akizindua mradi wa ufugaji samaki kutoka kikundi cha Bodaboda wilayani Kishapu kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi. Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog

Muonekano wa bwawa la ufugaji Samaki la kikundi cha Bodaboda wilayani Kishapu ambalo lipo jirani na mto Tungu wilayani Kishapu ambalo lina jumla ya Samaki 2,000 aina ya Kambale.

Mwenyekiti wa kikundi cha Bodaboda wilayani Kishapu Daniel Eva akielezea namna walivyopata wazo la kuanzisha mradi huo wa kufuga Samaki ili wapate kujikwamua kiuchumi.

Afisa uvuvi wilayani Kishapu Moses Zacharia akiwapongeza vijana hao wa Bodaboda namna wanavyoonesha juhudi za kuweza kujiajiri wenyewe na kujipatia kipato, na kuahidi Serikali kuendelea kushirikiana nao sambamba na kutoa ushauri namna ya kuuendeleza mradi wao huo wa ufugaji Samaki.

Meneja Miradi kutoka Shirika la REDESO Charles Buregela ambao wanajishughulisha shughuli za kuinua watu kiuchumi, akizungumza kwenye ufunguzi huo wa mradi wa Samaki, anasema bodaboda hao walifuata na kuomba msaada wa elimu hiyo ndipo wakawapatia pamoja na kuwa wezesha Nailoni ya kuhifadhia maji kwenye bwawa hilo, na kuahidi kuendelea kuwa unga mkono.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga Anthony Gwandu, akiwapongeza Bodaboda hao kwa kuanzisha mradi huo kujikwamua kiuchumi na kutoa wito kwa kuzitii Sheria za usalama barabarani ili fedha zao ziweze kuwa saidia katika maendeleo na siyo kuishia kulipa faini.

Askari wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga wakishuhudia mradi huo wa ufugaji samaki kutoka kikundi cha Bodaboda wilayani Kishapu.

Wananchi ,viongozi wilayani Kishapu na maaskari wa kikosi cha usalama barabarani wakiangalia mradi huo wa ufugaji Samaki.

Maaskari wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga wakiwa eneo la mradi wa ufugaji Samaki.

Mwenyekiti wa kikundi cha Bodaboda wilayani Kishapu Daniel Eva, akiomba pia Serikali iweze kuwaunga mkono katika mradi wao huo ili waweze kupanua wigo na kukua kiuchumi na taifa kwa ujumla.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga Anthony Gwandu, akiwasisitiza Bodaboda hao wawe na umoja, uaminifu kwenye kikundi chao na mtu ambaye ataonekana kuanza kuwa mjanja mjanja wamtoe kabla hajawavuruga, ili wapate kusonga mbele kimaendeleo.

Mwenyekiti wa mradi wa ufugaji Samaki Salumu Geogre akiwapatia chakula Samaki hao.

Bodaboda wakicheza muziki mara baada ya mradi wao wa ufugaji Samaki kuzinduliwa.

Bodaboda wakiondoka eneo la mradi tayari kwenda kucheza mpira wa miguu kati yao na Jeshi la Polisi katika uwanja wa shule ya Msingi Mhunze wilayani Kishapu.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga Anthony Gwandu akisalimiana na wachezaji wa Jeshi la Polisi kabla ya kuanza mtanange kati yao na Bodaboda.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga Anthony Gwandu akisalimiana na vijana wa Bodaboda kabla ya kuanza Mtanange kati yao na Jeshi la Polisi.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga Anthony Gwandu akiwa asa vijana wa Bodaboda na Askari Polisi kuwa mchezo wao uwe wa amani pamoja na kudumisha umoja kati yao na kusiwepo na chuki tena bali washirikiane pamoja kuijenga nchi pamoja na kutoa taarifa za waharifu ili mkoa ubaki kuwa salama na Amani.

Mchezo ukiendelea kuchezwa kati ya vijana hao wa Bodaboda wenye Jezi Nyeupe na Askari Polisi, ambapo Askari hao hadi dakika 90 zinakwisha waliibuka na ushindi wa goli moja lililofungwa na Philipo Michaeli kipindi cha pili.

Askari wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga wakiangalia mpira wa miguu kati ya Bodaboda na Polisi.

Mtanange ukiendelea kutazamwa.

Vijana wilayani Kishapu wakiangalia mpira wa miguu kati ya Bodaboda na Jeshi la Polisi.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga Anthony Gwandu akiangalia mtanange kati ya Askari Polisi na Bodaboda uliochezwa katika shule ya Msingi Mhunze wilayani Kishapu mara baada ya kumaliza kuzindua mradi wa ufugaji Samaki.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga Anthony Gwandu akimpongeza Philipo Michael ambaye alifunga Gori la kuwapatia ushindi Askari hao, kati ya mchezo wao na Bodaboda wilayani Kishapu.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga Anthony Gwandu mkono wa kulia akiingia ukumbini na mwenyekiti wa Bodaboda wilayani Kishapu Daniel Eva ,kwa ajili ya kusheherekea uzinduzi wa mradi huo wa ufugaji Samaki.

Wageni waalikwa pamoja na Bodaboda wakiwa ukumbi kusheherekea uzinduzi wa mradi wa ufugaji Samaki hafla iliyofanyika kwenye kumbi za Shirecu wilayani Kishapu.

Mwenyekiti wa kikundi cha Bodaboda wilayani Kishapu Daniel Eva akifungua Sherehe hiyo na kusema mikakati yao ya kujiendeleza kiuchumi ambapo pia wanatarajia kufungua eneo la kuoshea Magari pamoja na Pikipiki ili kupanua wigo wa kujikwamua kiuchumi.

Wenyeviti wa bodaboda Kahama na Manispaa ya Shinyanga nao wakijumuika na Bodaboda wilayani Kishapu kusherehekea uzinduzi wa mradi huo wa ufugaji Samaki.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga Anthony Gwandu akizungumza kwenye Sherehe hiyo na kuwataka Bodaboda wajitambue na kujituma katika kazi zao sambamba na kutii sheria za usalama barabarani na kuukataa uhalifu.

Bodaboda wakiwa ukumbini wakipata moja baridi moja moto.

Askari wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga nao wakiwa kwenye hafla hiyo ya Bodaboda wilayani Kishapu.

Burudani zikiendelea ukumbini ambapo Bodaboda wakicheza na wake zao huku wakisema wamechoka kuambiwa wanaongoza kwa vitendo vya kutia mimba wanafunzi na wakati wao wana wake zao.

Askari wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga nao wakiburudika na Bodaboda hao kwa kucheza Muziki.

Awali Bodaboda wilayani Kishapu wakiwa kwenye maandamano kwa ajili ya kumpokea mkuu wa kikosi cha usalama barabara mkoani Shinyanga Anthony Gwandu kwa ajili ya kwenda kuzindua mradi wao wa ufugaji Samaki aina ya Kambare ambao utawainua kiuchumi.

Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post