BERNARD MEMBE AIBUKIA KANISANI MISA YA KRISMASI

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali ya awamu ya nne, Bernard Membe amekuwa miongoni mwa waumini wa dini ya kikristo walioshiriki ibada ya Krismasi katika kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam.

Membe ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Mtama, ameshiriki misa hiyo leo Jummane Desemba 25, 2018 iliyoongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa.

Katika ibada hiyo, Membe ambaye hivi karibuni alizua gumzo kati yake na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, alionekana kwenye safu ya mbele akiwa amevaali suti ya rangi nyeusi.

Membe alikuwa gumzo hivi karibuni baada ya Dk Bashiru kutamka hadharani kuwa waziri huyo wa zamani anakwamisha mikakati ya urais ya 2020.

Ibada hiyo ilikuwa ya pili na ilianza saa nne, baada ya ile asubuhi kuhudhuriwa na mke wa Rais Janeth Magufuli.

Akitoa mahubiri katika ibada hiyo, Askofu Nzigilwa amesema Sikukuu ya Krismasi ina neema ya matunda manne na ni vyema waumini wa dini wakayazingatia.

Amesema matunda hayo kuwa ni upatanisho, furaha, umoja na amani na kusema ni vyema waumini wa dini wakayatilia mkazo wakati wakisherehekea Krismasi.

“Tunaishi dunia yenye misuguano, kuna watu hawaongei katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya kazi tena wengine pia wanaishi nyumba moja halafu tunasema tunasheherekea Krismasi, sikukuu gani hiyo wakati hakuna upatanisho?” Alihoji Askofu Nzigilwa.

Na Bakari Kiango, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post