WANACHUO KORTINI KWA KUPOST PICHA ZA NGONO ZA MWANACHUO WALIYEMLAWITI GESTI DAR



Na Francisca Emmanuel - Habarileo

MWANACHUO wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Anna Mwaisumo (23) na mpenzi wake, Samson Kisuguta (28), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka manne likiwemo la kulawiti na kuchapisha picha za ngono kwenye mtandao wa kijamii wa WhatsApp.

Mwaisomo ambaye makazi yake ni kwenye Hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) huku Kisuguta akiishi mkazi wa Msasani na mfanyabiashara, walifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Salim Ally. 

Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono akisaidiana na Janeth Magohe alidai washitakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya mwaka 2017 na mwaka huu maeneo ya Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam.

Magohe alidai katika mashitaka ya kwanza kuwa, washitakiwa wote kwa pamoja katika tarehe na mahali kusikofahamika mwaka jana, ndani ya jiji hilo, walikula njama kutenda kosa la kulawiti, kuchapisha picha za ngono na kulazimisha kupata fedha ili kutochapisha picha hizo.

 Alidai katika mashitaka ya pili kuwa, Desemba 10, mwaka jana maeneo ya nyumba ya kulala wageni ya Morgan maeneo ya Msasani wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Kisuguta alimlawiti kinyume cha maumbile mwanafunzi anaesoma katika moja ya vyuo hapa nchini.

Katika mashitaka ya tatu, inadaiwa Oktoba 7, mwaka huu ndani ya jiji hilo, Mwaisomo pamoja na Kisuguta walichapisha picha za ngono kupitia ukurasa wa WhatsApp kinyume cha sheria. 

Pia alidai Novemba 13, mwaka huu, ndani ya jiji hilo, washitakiwa hao walimlazimisha mlalamikaji huyo kutoa fedha taslimu Sh 250,000 ili wasichapishe picha hizo.

 Washitakiwa hao walikana mashitaka na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika hivyo waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Ally alitaja masharti ya dhamana kuwa kila mshitakiwa atatakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoa serikali za mitaa watakaosaini bondi ya Sh 500,000 kila mmoja. 

Hata hivyo, washitakiwa hao walikosa dhamana baada ya kushindwa kutimiza masharti hayo na kurudishwa rumande hadi Januari 3, mwaka huu kesi itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Inadaiwa kuwa Mwaisumo alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mlalamikaji huyo wakati wakisoma sekondari ya juu na baada ya kuchaguliwa kujiunga na vyuo tofauti hawakuwa na mahusiano mazuri.

Inadaiwa baadaye mwanamke huyo (Mwaisumo) alimtafuta mlalamikaji na kutaka waonane ndipo walikutania kwenye nyumba ya kulala wageni, lakini baadaye wakati wakiwa huko, mwanamke huyo alitoka na kuingia tena na mwanamume mwingine ambaye ni Kisuguta.

 Hata hivyo, baada ya Kisuguta kuingia chumbani, alimlawiti kinyume cha maumbile mlalamikaji huku wakichukua video na baadaye walitumia picha hizo kulazimisha kupewa fedha na mlalamikaji ili wasizichapishe kwenye mitandao ya kijamii.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527