GARI LA MAZISHI LILILOTOLEWA NA NAIBU WAZIRI LAZUA GUMZO

Gari la kubebea maiti lililonunuliwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Anthony Mavunde, limeibua mjadala mkali kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii.

Mavunde ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM), alitoa gari hilo juzi na kulikabidhi kwa wananchi ili kila anayefiwa kwenye jimbo hilo alitumie bila malipo kwa ajili ya shughuli ya maziko.

Gari hilo aina ya Isuzu lililonakshiwa vizuri limeandikwa kwa herufi kubwa mbele kwamba gari la mazishi limenunuliwa na Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde.

Ingawa baadhi ya waliochangia walisema nia ya Waziri Mavunde ni njema, wengine waliokuwa wakichangia kwenye mitandao ya kijamii walihoji mbunge kuwapa wananchi gari la kubebea maiti badala ya kuweka utaratibu wa kuwatibu wanapougua ili wasife.

Wakati akikabidhi gari hilo juzi, Mavunde alisema alichukua uamuzi wa kununua gari hilo baada ya wananchi wengi kufika ofisini kwake mara kwa mara kuomba fedha za kuwasafirisha wapendwa wao wanapofariki dunia kutoka hospitalini kwenda kwenye mazishi.

Baadhi ya wachangiaji kwenye mitandao ya kijamii walihoji kama hicho ndicho kipaumbele cha wananchi wa jimbo la Dodoma Mjini huku wengine wakipongeza hatua hiyo kuwa itasaidia wananchi.

Siku moja kabla ya uzinduzi wa gari hilo, Mavunde alitumia ukurasa wake wa Facebook kuwakaribisha wananchi kushiriki uzinduzi huo na ndipo alipoanza kupata mashambulizi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527