Picha : SHIRIKA LA INTRAHEALTH LAWAPIGA MSASA WA TOHARA WAANDISHI WA HABARI MIKOA SABA

Shirika la IntraHealth International Inc. limeendesha mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka Mkoa wa Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Kagera na Kigoma katika mradi wa utoaji wa huduma za tohara kwa wanaume ikiwa ni afua mojawapo ya kuzuia maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI. 

Akifungua mafunzo hayo ya siku nne ambayo yameanza leo Desemba 10 hadi 13 mwaka huu,Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt. Japhet Simeo amesema vyombo vya habari vina nafasi kubwa kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa tohara kwa wanaume.

Alisema kampeni ya kuamsha ari ya upimaji wa VVU iliyofanyika mwaka 2017 mkoani Geita iliwafikia wakazi kwa asilimia 87 na kubaini kwamba wanaume ambao hawajatahiriwa wapo kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi ya VVU kuliko wale waliotahiriwa. 

“Tafiti zinaonyesha mwanaume ambaye hajapatiwa tohara yupo kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi ya VVU kuliko yule aliyefanyiwa tohara ambapo yeye anakuwa amepunguza uwezekano wa asilimia 60 kupata maambukizi”, alisema Japhet. 

Alisema mkoa wa Geita unakabiliwa changamoto ya kasi ya mambukizi mapya ya VVU kutokana na mila na desturi zilizopo ikiwemo wanaume kutofanyiwa tohara kwa kuhofia kupunguza nguvu za kiume. 

Kwa upande wake, mshauri wa huduma za tohara Mkoa wa Geita Dkt. Peter Sewa alisema licha ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii lakini wana mpango wa kuanza kutahiri watoto wenye umri wa umri wa siku moja hadi miezi miwili  mkakati ambao utawasaidia wanaume katika hatari ya maambukizi ya VVU na UKIMWI. 

“Tuna mpango wa kuanzisha huduma ya utoaji tohara kwa watoto wachanga ambapo kimsingi tumeanza mchakato huo ili kufikia malengo ya  kuwafikia wanaume ambao hawajapatiwa tohara”,alisema Dkt. Sewa. 

Shirika la IntraHealth International kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania linatekeleza mradi wa huduma za tohara kinga kwa wanaume kama afua mojawapo ya kuzuia maambukizi ya VVU katika mikoa saba kwa ufadhili wa mfuko wa Rais wa Marekani wa kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI(VVU) PEPFAR kupitia CDC.

Mradi huo unaotekelezwa kuanzia 2016-2021,kwa ushirikiano wa karibu na ofisi ya Rais-TAMISEMI,wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto,mpango wa taifa wa kudhibiti maambukizi ya UKIMWI(NACP) pamoja na kamati za usimamizi na uendeshaji wa huduma za afya mikoa na wilaya.

Tazama picha hapa chini
Mshauri wa huduma za tohara mkoa wa Geita Peter Sewa akieleza mikakati ya huduma za tohara ambapo amesema kutokana na muamko mdogo kwa jamii mkoa umejipanga kuanza kuwafanya tohara kwa watoto walio na umri wa kuanzia mwaka sifuri hadi miaka kumi na kuwaomba wazazi,walezi na jamii kwa ujumla kuthamini huduma ya tohara kwasababu husaidia kwa karibu asilimia 60 ya kutopata maambukizi ya virusi vya UKIMWI na magonjwa ya zinaa.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita,Dkt. Japhet Simeo akizungumza wakati wa akifungua mafunzo kwa waaandishi wa habari kutoka mikoa saba,pamoja na mambo mengine mganga huyo alisema vyombo vya habari vina nafasi kubwa kubadili mila na desturi ambazo zimepitwa na wakati kuhusu huduma ya Tohara.
Mafunzo yakiendelea. 
Mwezeshaji wa mafunzo Temigunga Mahondo akitoa mfano wa data zinazoonesha kiwango cha maambukizi ya VVU nchini.
Washiriki wakichangamsha bongo zao baada ya kupata mafunzo kuhusu umuhimu wa tohara kwa wanaume,hapo wanajaribu kuchora picha ya mtu.
Waandishi wa habari washiriki, wakiandika dondoo muhimu kuhusu tohara kwa wanaume. 
Washiriki kutoka mikoa ya Geita,Mwanza,Simiyu,Kagera,Kigoma,Mara na Shinyanga wakiwa ukumbini.
Mwezeshaji kutoka shirika la IntraHealth Temigunga Mahondo akieleza faida za tohara kwa wanaume na kuwakumbusha waandishi wa habari kutumia data wakati wa uandaaji wa habari ili kuongeza uaminifu kwa jamii lakini pia mamlaka kujua ukubwa na udogo wa tatizo husika.
Afisa habari mkoa wa Geita akifuatilia dondoo zinazotolewa na mwezeshaji ambapo kwa nafasi yake amewataka waandishi wa habari kuwa na mazoea ya kuibua changamoto za kiafya katika jamii ili ziweze kutatuliwa na mamlaka husika.
Mwezeshaji Temigunga Mahondo akiendelea kutoa mafunzo na kubadilishana mawazo na waandishi wa habari.
Mwandishi wa majukwaa ya habari za kimataifa Mweha Msemo akifuatilia mada ukumbini.
Mwandishi wa habari wa Radio Free Afrika Frankius Cleophace (wa kwanza kushoto),Mshauri wa huduma za tohara mkoa wa GeitaPeter Sewa  (wa pili kushoto) akifuatiwa na Mary Mndeme  kutoka kitengo cha habari na mawasiliano IntraHealth wakiwa ukumbini.
Mwandishi wa habari wa Radio one na ITV Mkoa wa Mwanza Mabere Makubi amekula pozi huku akifuatilia mafunzo ya tohara.
Mwandishi wa habari Clouds media Shinyanga,Kasisi Kosta  akifuatilia mada.

Picha zote na Malaki Philipo Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post