MKUU WA WILAYA AKANUSHA MADAI YA KUFANYA UDHALILISHAJI.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobasi Katambi, amekanusha madai ya kudhalilisha baadhi ya watuhumiwa waliokuwa wakikamatwa kupitia operesheni maalum ambayo ilikuwa ikiendeshwa na ofisi yake pamoja na ofisi ya Mkuu wa Polisi mkoani Dodoma, Kamanda Gilles Muroto.

Viongozi hao wawili walikuwa wakiendesha kampeni ya kuwakamata watu wanaojihusisha na matumizi ya madawa ya kulevya pamoja na matukio mengine ya kiuhalifu na baadaye kuyaonesha kwa umma hali inayodaiwa kuwahukumu watu hao kabla ya kufikishwa mahakamani.

Akijibu madai hayo Mkuu wa huyo Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobasi Katambi, amesema "kuhusu suala la uhalifu, hata mimi DC naweza kukamatwa kwa hiyo sio kwamba tunawadhalilisha bali ni kujaribu kuhakikisha wanapata haki zao au kumrejesha kwenye maadili ya kijamii."

"Ukimkuta mtu mtaani anafanya uhalifu, na ukikuta watu wanazungumza kwamba tunawadhalilisha kwa kweli hawana nia njema na jamii yetu, ndiyo maana sisi tunachofanya tunawaonesha ili waweze kurudi kwenye jamii kama watu safi," amesema Katambi.

"Kuhusu neno watapata tabu sana, tunamaanisha atakayevunja sheria lazima akamatwe na afikishwe mahakamani ili akakutane na hiyo tabu, na yeyote atakayeivunja hiyo lazima achukuliwe hatua za kisheria, wakidai tumeshahukumu sio sawa," ameongeza Katambi.

Patrobas Katambi aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA, kabla ya baadaye kutangaza kujiunga na Chama cha Mapinduzi CCM kwa madai ya kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli na mwezi July 2018 alichaguliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini.
Chanzo: Eatv

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527