SAKATA LA MEMBE NA BASHIRU LAZIDI KUKOLEA...CCM YATOA TAMKO TENA

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewaonya watu wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kuweka habari za uongo zinazowahusu viongozi wa chama hicho tawala.

Pia, kimesema Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally hana akaunti ya mtandao wa kijamii wa Twitter.

Chama hicho tawala kimetoa taarifa yenye ufafanuzi huo  Jumatano Desemba 5, 2018 ikiwa ni siku moja tangu Dk Bashiru Ally kukanusha taarifa za mtandaoni zilizomnukuu akimjibu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole inaeleza kuwa watu wanaotumia vibaya mitandao ya jamii wana lengo la kuleta taharuki.

“Kuna akaunti ya mtandao wa Twitter yenye jina la Bashiru Ally na inatoa kauli ambazo sio zake,” inaeleza taarifa hiyo.

“Jana katika mitandao ya kijamii watu wenye hila, fitna, husuda na kila chembe ya uzandiki wametengeneza kauli ya kubeza, potofu na isiyo na ukweli kuwa Bashiru Ally amemjibu kiongozi mstaafu, mwanachama wa CCM na kada mwenzetu mzee Pius Msekwa,” imeongeza.

Mbali na hayo, Polepole amesema kulikuwa na upotoshwaji wa taarifa za chama hicho iliyodai kuwepo kwa mkutano wa wanahabari katika ofisi ndogo za makao makuu ya CCM Lumumba Dar es Salaam.

“Utaratibu wa CCM msemaji ni mmoja naye ni mwenyekiti, kwa niaba ya chama anayekasimiwa dhamana ya kusema ni Katibu wa halmashauri kuu ya Taifa, mwenye dhamana ya itikadi na uenezi na si vinginevyo,” amesema Polepole.

Polepole amezitaka mamlaka zinazohusika kuchunguza na kuchukua hatua zinazostahili kwa watu wanaotumia vibaya mitandao ya jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527