CCM ARUSHA WAKUTANA KUMPONGEZA RAIS MAGUFULI KWA KUFUTA KIKOKOTOO


Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa Arusha kimempongeza Rais John Magufuli kwa utendaji wake mzuri katika kipindi cha miaka mitatu ikiwemo kurejesha kikokotoo cha zamani cha mafao ya wafanyakazi.

Wakitoa tamko lao leo Jumamosi Desemba 29, 2018 katika mkutano uliofanyika ukumbi wa CCM mkoa wa Arusha na kuwashirikisha wanaccm kutoka wilaya zote tano za mkoa wa Arusha, wamesema Rais John Magufuli ndiye mzalendo wa kweli.

Akitoa salamu kwa niaba ya wabunge wa mkoa Arusha, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha ambaye pia ni mbunge wa Ngorongoro amesema katika kipindi cha miaka mitatu Rais Magufuli amefanya kazi ya mfano.

Ole Nasha amesema ndani ya miaka mitatu, Rais Magufuli amenunua ndege, amejenga madarasa na vivuko, ameanza ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es salaam hadi Dodoma.

"Sio haya tu Rais wetu ameanza mradi mkubwa wa umeme wa Stiglers Gorge na jana amefanya kubwa kutetea wafanyakazi kurejesha kikokotoo cha zamani," alisema.

Mkuu wa wilaya ya Arusha, Gabriel Daqaro amesema, kazi alizofanya Rais ni kubwa na inawahakikishia CCM ushindi mwaka 2020.

Katika mkutano huo uliokuwa unaongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha, Loota Sanare pia ulihudhuriwa na mkuu wa mkoa Arusha Mrisho Gambo, wabunge na madiwani.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post