ALI KIBA KUANZA NA MBEYA CITY MWISHONI MWA JUMA

Mchezaji wa klabu ya Coastal Union ambaye ni msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Ali kiba amezungumzia juu ya ukamilifu wake kwa sasa na klabu kwa ujumla kuelekea mchezo dhidi ya Mbeya City mwishoni mwa juma hili.


Alikiba ambaye hajacheza mchezo wowote wa ligi kuu Tanzania bara mpaka sasa kwenye klabu yake, amekiri kuwa sasa yuko fiti kurudi dimbani kwenye mchezo huo ambao Coastal Union itashuka dimbani dhidi ya Mbeya City.


Akizungumza katika mazoezi kuelekea mchezo huo, Alikiba amesema, "Mpaka sasa hivi niko tayari, niko mazoezini takribani wiki nzima sasa, wachezaji tumeshazoeana na tumeshajua mfumo gani tunacheza. Na haitokuwa ngumu sana kwa mchezaji kama mimi ambaye nina uzoefu na mambo ya mpira kwa muda mrefu, kwahiyo niko tayari,".


Naye kocha wa klabu ya Coastal Union, Juma Mgunda amesema kuwa kikosi chake kiko imara wakati wote na kukanusha vikali taarifa za kuingiliwa katika maamuzi ya upangaji wa kikosi na viongozi wa klabu hiyo.


"Mimi sikuja hapa kupigiwa kura, nimekuja kwasababu najua kufundisha mpira na nimesomea kufundisha, kwahiyo hatatokea na haiwezi kutokea nikapangiwa kikosi. Huyu Alikiba munayemuona, anafanya vizuri sasa katika mazoezi na mwisho wa yote atapata nafasi atacheza," amesema Juma Mgunda.

Chanzo:Eatv

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post