Mkazi wa Kijiji cha Nakayaya, wilayani Tunduru mkoani Ruvuma Awetu Makunula (44), amejinyonga hadi kufa kwa madai ya kuchoka kusumbua wanafamilia kutokana na hali ya afya yake.
Taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa Makunula alikutwa akining`inia juu ya mti wa mkorosho jirani na nyumba ya wazazi wake, mjini hapa.
Mume wa marehemu Makunula, Salum Namtikwe, alisema kuwa usiku walilala wote na kabla ya tukio hilo aliamka majira ya saa 11 alfajiri na kumuaga kuwa anatoka nje kwa ajili ya kufagia nje ya nyumba yao ili amalize shughuli hiyo mapema na kwenda shambani.
Alisema baada ya kupewa maelezo hayo yeye aliendelea kulala, lakini baadaye alishangaa kupata taarifa za mkewe kukutwa akiwa amejinyonga hadi kufa baada ya kujining`iniza katika mti uliopo jirani na nyumbani kwa wazazi wake.
Alisema baada ya kupatiwa taarifa hizo aliamka na kwenda eneo la tukio na kumtambua marehemu na baadaye walitoa taarifa kwa viongozi wa serikali kwa ajili ya taratibu za kuuondoa mwili huo katika eneo hilo.
Aidha, akisimulia maisha ya mkewe, alisema kabla ya tukio hilo alikuwa akisumbulia na maradhi mbalimbali mara kwa mara jambo ambalo lilikuwa likimnyima amani wakati wote.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, ASCP Gemin Mushy, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kusema polisi inaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo hicho.
Kamanda Mushy, alisema katika tukio hilo mwanamke huyo alijinyonga kwa kutumia mtandio alio jifunga shingoni na upande mwingine kuufunga juu ya mti wa mkorosho.