AGAPE : MIMBA NA NDOA ZA UTOTONI ZINACHANGIA MAAMBUKIZI YA VVU...; DAS 'MSIOGOPE KUPIMA'


Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga,Boniface Chambi akikabidhi sare za shule zilizotolewa na shirika la Agape kwa ajili ya watoto yatima/wanaoishi katika mazingira wanaosoma katika shule ya msingi Pandagichiza wakati wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
****
Jamii imetakiwa kupiga vita mila potofu, mimba na ndoa za utotoni kwani zinachangia uwepo wa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa vijana na watoto mkoani Shinyanga.

Rai hiyo imetolewa leo Jumamosi Desemba 1,2018 na Afisa Mradi wa Afya ya Uzazi na Ujinsia kwa Vijana wa Shirika la Agape AIDS Control Program la Mjini Shinyanga Lucy Maganga wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani ambapo katika wilaya ya Shinyanga yamefanyika katika kijiji cha Shilabela kata ya Pandagichiza.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga,Boniface Chambi kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Jasinta Mboneko.

Maganga alisema ili kutokomeza Maambukizi ya VVU ni lazima jamii ipewe elimu ya afya uzazi na madhara ya mila potofu, mimba na ndoa za utotoni kwani vinachangia maambukizi ya VVU na Ukimwi hasa kwa vijana na watoto.

Alisema katika kuhakikisha maambukizi ya VVU kwa watoto yanatokomezwa mkoani Shinyanga,shirika la Agape limekuwa likitoa elimu ya afya uzazi kupitia mradi wake wa wa Afya ya Uzazi na Ujinsia kwa Vijana katika wilaya ya Shinyanga.

Maganga alisema lengo la mradi huo unaotekelezwa na Agape kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Sida la nchini Sweden, ni kuwajengea uwezo watoto na vijana kujitambua,kujithamini na kujitunza dhidi ya tabia hatarishi zinazoweza kuwasababishia mimba za utotoni na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi pamoja na magonjwa ya zinaaa.

“Tupo hapa kuungana na wadau wengine kuadhimisha siku ya Ukimwi Duniani kwani, kwetu Ukimwi ni suala mtambuka,Ukimwi upo, siku ya leo inatukumbusha kuwa ni jukumu letu sote kujilinda na kuwalinda wengine dhidi ya maambukizi ya VVU”,alieleza Maganga.

“Katika kuadhimisha siku ya Ukimwi duniani mwaka huu,Agape tumetoa elimu kuhusu VVU na Ukimwi kwa njia ya sinema katika vijiji vya kata ya Shilabela,Sayu na Pandagichiza tukilenga makundi yote katika jamii wakiwemo watoto na vijana”,alisema.

Kwa upande wake,Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga,Boniface Chambi aliwataka wananchi kutoogopa kupima na kutumia ARVs hivyo wajitokeze kupima afya zao ili kuhakikisha malengo ya 90 tatu yanafikiwa.

“Tunataka ifikapo 2020, asilimia 90% ya watu wenye maambukizi ya VVU wawe wamefikiwa na kupimwa,kati yao asilimia 90% ya walioathirika watapewa dawa za kufubaza virusi (antiretroviral treatment) na asilimia 90% ya watakaotumia dawa hizo hawataweza kuwaambukiza wenza watakaojamiiana nao kwasababu virusi vitakuwa vimefubazwa na tiba hiy”,alisema Chambi.

Naye Mganga Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Dkt.Amos Mwenda alisema wanaendelea kushirikiana na wadau waliopo katika halmashauri hiyo ili kuongeza nguvu kwenye huduma za upimaji VVU,uanzishaji wa dawa za kufubaza VVU na kutoa huduma stahiki kwa watu waishio na VVU.

Hata hivyo alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni ushiriki duni wa jamii hasa wanaume katika suala la upimaji VVU na huduma ya afya ya baba,mama na mtoto pamoja na upungufu wa wataalamu wa afya kwa ajili ya utoaji huduma shirikishi za UKIMWI.

Shirika la Agape limetumia fursa ya maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani kutoa msaada wa sare za shule kwa wanafunzi yatima 10 wanaosoma katika shule ya msingi Pandagichiza kwa ajili ya kuwapa hamasa wapende shule na kufanya vizuri kwenye masomo yao.

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA
Mgeni rasmi Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga,Boniface Chambi kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Jasinta Mboneko akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani wilaya ya Shinyanga ambayo yamefanyika katika kijiji cha Shilabela kata ya Pandagichiza.Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Afisa Mradi wa Afya ya Uzazi na Ujinsia kwa Vijana wa Shirika la Agape AIDS Control Program la Mjini Shinyanga Lucy Maganga akizungumzawakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani ambayo katika wilaya ya Shinyanga yamefanyika katika kijiji cha Shilabela kata ya Pandagichiza.

Wanafunzi na wananchi wa Pandagichiza wakiwa kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani Desemba 1,2018.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Ngasa Mboje akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani katika wilaya ya Shinyanga.
Mganga Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Dkt.Amos Mwenda akisoma taarifa kuhusu maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani Desemba 1,2018.
Mgeni rasmi Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga,Boniface Chambi kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Shinyanga,Jasinta Mboneko akikabidhi sare za shule kwa mmoja wa wanafunzi/watoto yatima 10 wanaosoma katika shule ya msingi Pandagichiza iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.Sare hizo zimetolewa na Shirika la Agape ambalo linatekeleza Mradi wa Afya ya Uzazi na Ujinsia kwa Vijana katika halmashauri hiyo. 
Mwanafunzi wa shule ya msingi Pandagichiza akipokea sare ya shule.
Wanafunzi wa shule mbalimbali katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakisubiri kupewa zawadi mbalimbali ikiwemo ya sare za shule,madaftari na kalamu.
Katibu Tawala wilaya ya Shinyanga,Boniface Chambi akikabidhi zawadi ya madaftari na kalamu kwa mwanafunzi.
Wadau mbalimbali wakiwa kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani Desemba 1,2018.
Wanafunzi na wananchi wa Pandagichiza wakiwa kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani Desemba 1,2018.

Wanafunzi wa shule ya msingi Pandagichiza wakifurahia zawadi ya sare za shule walizopewa na shirika la Agape.Kulia ni Mwalimu wa shule hiyo,Lucia Maungo.
Wanafunzi wanaosoma katika shule ya msingi Pandagichiza halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakiwa wameshikilia zawadi ya sare za shule zilizotolewa na shirika la Agape.
Wanafunzi wanaosoma katika shule ya msingi Pandagichiza halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,walimu wa shule ya msingi Pandagichiza na wafanyakazi wa shirika la Agape wakiwa katika picha ya pamoja.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527