WATU 25 WADAIWA KUUAWA NA WAASI WA ADF NCHINI DRC

Watu 25 wameuawa katika mashambulizi mawili yanayoaminika kutekelezwa na kundi la waasi la Allied Democratic Forces, ADF, katika mtaa wa Beni, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC).


Idadi ya waliouwawa eneo la Mangolikene, nje kidogo ya mji wa Beni, Kivu kaskazini, imeongezeka na kufikia 20. Watu wengine 5 waliuwawa katika kijiji cha Paida karibu na Beni ameeleza mwandishi wa VOA.

Mwandishi huyo mjini Goma ameeleza kuwa mashambulizi hayo yalitokea usiku wa kuamkia Ijumaa.

Nyumba kadhaa zilichomwa moto na kuna taarifa kwamba baadhi ya watu wametekwa nyara na kikundi cha watu waliowashambulia.

Wakaazi wanasema kwamba waliowashambulia walikuwa wamevalia sare za kijeshi na walikuwa wanazungumza Kilingala.

Msemaji wa jeshi katika sehemu hiyo Kapteni Mak Hazzukay, amesema kwamba mauaji yametokea baada ya waasi kushambulia kambi ya jeshi.

Serikali ya DRC imekuwa ikilaumu kundi la ADF kwa mauaji, wizi wa kitumia nguvu na utekaji nyara, lakini wakati mwingine taarifa kamili hukosekana kuhusu wanaofanya mashambulizi. Kundi la ADF, kutoka Uganda, limeuwa mamia ya watu tangu mwaka 2014.

Mashambulizi ya leo yanajiri siku moja baada mgombea wa urais Martin Fayulu, mmoja kati ya wagombea wengine wa urais, kuzindua kampeni zake katika mji wa Beni. DRC inajiandaa kwa uchaguzi mkuu desemba 23.

Chanzo:Voa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post