WASHUKIWA SITA WA UJAMBAZI WAUAWA DAR...WAFUASI WA FDD NDD WAHUSISHWA

Watu 6 wakiwemo Raia wa Burundi na wafuasi wa kikundi cha waasi cha FDD NDD cha nchini humo, wameuawa wakati wakitekeleza tukio la ujambazi jijini Dar es salaam ambapo silaha za kivita na risasi zimekamatwa.

Taarifa hiyo imetolewa leo Novemba 29 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa wakati akiwasilisha ripoti ya matukio ya uhalifu kwa kipindi cha wiki moja.

Kamanda Mambosasa amesema  Jeshi hilo limefanikiwa kumkamata jambazi sugu ambaye amewahi kutekeleza matukio mengi ya uhalifu na kuua raia kadhaa wakiwemo Polisi katika mikoa mbalimbali nchini.

"Watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kuwepo kwa matukio ya uhalifu yaliyotokea huko Mabibo External, ambapo mfanyabiashara wa TIGOPESA/MPESA aliporwa shilingi milioni 50 na huko, Tegeta mfanyabiashara raia wa China ambaye aliporwa shilingi milioni 10", amesema Mambosasa.

Imeelezwa kuwa matukio mengine waliyoshiriki ni pamoja na kuteka mgodi wa Tulawaka Geita mwaka 2011, kuvamia maduka ya kubadilishia fedha za kigeni huko Zanzibar, Mwaka 2012 walivamia kituo cha mafuta mkoani Kagera na kufanya mauaji, Pia walivamia maduka yaliyopo karibu na kituo cha Polisi Chato na hivyo kukishambulia kituo ili kurahisisha uporaji.

Chanzo:Eatv

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527