SERIKALI : HAKUNA UTHIBITISHO WA KISAYANSI KUWA KUKU WA KISASA WANASABABISHA WANAUME KUOTA MATITI NA WANAWAKE KUOTA NDEVU

Serikali imesema hakuna uthibitisho wa kisayansi kuwa madawa na vichochezi vya ukuaji wa kuku na mayai ya kisasa yanasababisha wanawake kuota ndevu na wanaume kuota matiti.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum(CUF), Zainab Mndolwa Amir.


Katika swali lake, Mbunge huyo alisema ziko aina mbili za ufugaji ambazo ni wa kienyeji na ufugaji wa kisasa.


"Ufugaji wa kuku wa kisasa hutumia dawa nyingine sana katika ukuzaji na hutumia muda wa wiki tatu hadi nne kutumiwa na binadamu. Je, kuku hao wana madhara gani kwa binadamu," alihoji.


Pia alihoji serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wafugaji wa kuku kutumia njia bora ya kisasa ambayo haina mashaka kwa watumiaji.


Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri Ulega alilihakikishia bunge kuwa, ulaji wa nyama ya kuku wa kisasa au mayai ya kuku wa kisasa hauna madhara.


Aidha, alisema ufugaji wa kuku wa kisasa hauendani na matumizi ya dawa kwa wingi.


Alisema vyakula vinavyotumika kulisha kuku wa kisasa huwa na viini lishe kama madini, vitamin, protini, na nishati pamoja na chanjo ambazo sio dawa na ni muhimu kwa ukuaji na afya ya kuku na havina madhara kwa afya ya mlaji.


Hata hivyo, alisema ukuaji wa haraka wa kuku wa kisasa unaofanya kuwa tayari kwa matumizi ndani ya kipindi kifupi cha wiki nne mpaka sita hutokana na ulishaji wa vyakula vyenye ubora pamoja na kuwapo kwa vinasaba kwa ukuaji wa haraka na siyo matumizi ya dawa au vichocheo.


"Pia hakuna uthibitisho wa kisayansi wa dawa na vichochezi kusababisha ukuaji wa haraka wa kuku," alisema.


Ulega alisema serikali imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji wa kuku kudhibiti vimelea vya magonjwa ili kupunguza matumizi ya dawa katika ufugaji wa kuku wa kisasa.


Alitaja baadhi ya mikakati kuwa ni pamoja na kusajili na kusimamia mashamba ya kuku wazazi, na vituo vya kutotolesha vifaranga ili kuzalisha wasio na magonjwa, kushirikiana na wadau kuendesha mafunzo kwa wafugaji kuhusu ufugaji wa kuku unaozingatia usalama wa mazingira na mbinu za ufugaji bora wa kuku.


Ulega alisema pia serikali inaendelea na mkakati wa kusimamia na kusajili utengenezaji wa vyakula vya kuku vyenye ubora ili kupunguza usambazaji wa vyakula vyenye vimelea vya magonjwa.


"Serikali inasimamia Sheria ya Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama Na 13 ya mwaka 2010 na kanuni zake zinazokataza matumizi ya dawa na vichocheo kwenye vyakula vya kuku ili kulinda afya ya walaji," alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post