MUSWADA WA MAREKEBISHO YA VYAMA VYA SIASA WASOMWA KWA MARA YA KWANZA BUNGENI

Muswada wa Marekebisho ya Vyama vya Siasa wa mwaka wa fedha 2018 umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni leo Ijumaa Novemba 16, 2018.

Katika muswada huo miongoni mwa mambo yanayopendekezwa ni kuongezwa kwa kifungu ambacho kitamwezesha Msajili wa Vyama vya Siasa kusitisha usajili wa chama cha siasa kitakachovunja masharti ya sheria.

Muswada huo umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni ambapo Mwenyekiti wa Bunge Andrew Chenge amesema Spika wa Bunge, Job Ndugai ataipangia Kamati ya Bunge itakayofanya uchambuzi.

“Kifungu cha 19 kinapendekezwa kurekebishwa ili kumwezesha msajili wa vyama vya siasa kufuta usajili wa chama cha siasa kitakachobainika kuwa kilipata usajili kwa njia zisizo za halali,” sehemu ya sababu ya muswada huo imesema.

Pia, muswada huo unalenga katika kuzuia viongozi wa vyama vya siasa kutokuwa wajumbe wa bodi ya wadhamini.

“Muswada pia unapendekeza kufuta kifungu cha 21A na kifungu cha 21B kinapendekezwa kufanyiwa marekebisho ili kuliwezesha Baraza la Vyama vya Siasa kupata fedha kutoka katika bajeti ya Serikali na wafadhili,” amesema.

Muswada huo unapendekeza pia kuongezwa kwa vifungu ili kuainisha makosa na adhabu na kusitishwa kwa usajili wa vyama vya siasa vitakavyokiuka masharti ya sheria.

Pia, inapendekeza kufanyiwa marekebisho ili kumpa mamlaka waziri mwenye mamlaka ya kutengeneza kanuni za uandaaji wa taarifa za hesabu za vyama vya siasa na mambo yatakayojumuishwa katika katiba za vyama vya siasa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post