SERIKALI HAIJAWEKA UKOMO WA IDADI YA WATOTO WA KUZAA

SERIKALI imesema haijaweka ukomo wa idadi ya watoto wa kuzaa kwa wananchi wake na badala yake wazae idadi ambayo wataweza kumudu kuwapatia mahitaji yote muhimu.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Dk Faustine Ndungulile wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Suzan Limo (Chadema),

Katika swali lake, mbunge huyo alisema Serikali imetoa mwongozo wa kuondolewa kwa uzazi wa mpango baada ya kauli ya Rais kutaka wananchi wazae bila ukomo,

‘’Nini kauli ya Serikali uzazi wa mpango uwepo au kuondoa na kuacha watu wazae watakavyoweza?” alihoji.

Akijibu swali hilo, Naibu waziri huyo alisema hakuna mwongozo wowote uliotolewa na Serikali wa kuondoa uzazi wa mango.

Dk. Ndungulile alifafanua kuwa hoja ya rais haikulenga kusitisha uzazi wa mpango bali alitaka watu wazae kulingana na uwezo wao.

‘’ Kila mtu anatakiwa kuzaa huku akijua anatakiwa kuwa na uwezo wa kuwapatia mahitaji muhimu kama vile chakula na elimu na huduma nyingine za binadamu na sio vinginevyo’’ alisema.

Akiongeza majibu ya swali hilo, Mwenyekiti wa Bunge Najma Giga alisema: ‘’ Hata katika vitabu vya dini vimesema kuwa zaeni muongezeke muijaze dunia, hivyo kauli ya Rais ipo sahihi na majibi ya Serikali pia sahihi’’.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto ( CCM) alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha k mkakati wa taifa wa kupunguza vifo vya wanawake na watoto wa mwaka 2016 hadi 2020 unatimia.

“Tanzanai inakusudia kuongeza matumizi ya njia ya kisasa ya uzazi wa mpango kutoka asilimia 32 ya mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 45 ifikapo 2020.

“Vilevile kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 ya mwaka 2015 hadi 292 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo 2020,

Akijibu swali hilo, naibu waziri alisema wizara inatekeleza mkakati wa pili wa kuboresha huduma za afya uzazi, mama, watoto na vijana wa mwaka 2016 hadi 2020.

‘’ Mkakati huu umujikita zaidi kutekeleza malengo endelevu ya maendeleo ( SDGs) duniani na mkakati wan ne wa sekta ya afya,’’ alisema.

Alisema mkakati huo umeeleza bayana kuwa ili kupunguza vifo inahitaji kuhamasisha matumizi ya uzazi wa mpango , matumizi mazuri ya wataalam wa uzazi (wakunga na madaktari).

Pia alisema uwepo wa huduma za dharura za uzazi na mtoto mchanga na kuwa na mazingira yaliowezeshwa katika utoaji huduma.

Hata hivyo alisema wizara yake imeendelea kuboresha huduma bora ya dharula za uzazi na mtoto mchanga zenye uwezo wa kufanya upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni, kwa kuzisogeza karibu na wananchi.

Alisema katika kuhakikisha hilo linafanikiwa tayari ujenzi na ukarabati wa vituo 208 unaendelea nchi nzima.

Chanzo-Mtanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527