ROSE MUHANDO,KONDOO ALIYETENGWA NA WACHUNGAJI

Miaka ya 2000 mwanzoni. Natoka Moro kurudi Dar. Kilichonipeleka huko ni shoo ya Joseph Mbilinyi ‘Sugu’. Akiwaaga mashabiki wa Moro baada ya kutangaza kuachana na muziki. Kwa kile alichodai kutaka kujikita kwenye biashara. Uamuzi huu ulishitua watu.

Kwenye ubora wake analisusa game? Watu hawakuamini. Daslama yote ilidondoka Moro. Ndani ya ukumbi wa Mango Park. Kila ukigeuka unakutana na sura za watoto wa Kino, Sinza, Ilala. ‘Masista Duu kwa Mabrazameni’ waliiteka Moro usiku mzima.

Hakuacha muziki kwa mapenzi yake kabla ya kurejea tena kwa kishindo. Kulikuwa na mazingira ya chuki kwa wadau wakubwa wa muziki wakati ule dhidi yake. Ndo maana hakutaka kuondoka bila kuaga watu aliokaa nao muda mrefu (mashabiki). Chuki zinaua sanaa.

Vurugu za usiku ule. Mitungi mingi na hofu ya vijana kulala peke yao. Kulipokucha tulikuwa hoi kwa uchovu. Baada ya supu tu, urafiki na udongo mwekundu wa Moro ulikufa. Safari ya kurejea Dar ikaanza nikiwa na Kebby na Jerry. Kawaida safarini watu hutekwa na ngoma za dini.

Hii safari ilinipa nafasi nzuri ya kumfahamu dada mwenye sauti ya pekee. Pumzi na mizuka ya kutangaza neno la Mungu kwa nyimbo. Nilimsikiliza kuanzia Mikese mpaka Ubungo. Nikamuelewa na nikahusudu uwezo wa Rose Muhando.

Kuanzia hapo si mimi tu. Wabongo wakamuelewa. Wakampenda. Mpaka nje ya mipaka yetu. Kimbiza sana waimbaji wenzake kwa shoo. Wingi wa mashabiki na mauzo ya albamu. Kila tamasha hakukosa. Msama anamuachaje Rose?

Rose wa sasa si yule tena. Kawa yeyote. Thamani yake inabaki kwenye ubinadamu kama binadamu. Ule ubora uliofanya waumini na viongozi wa dini mbalimbali kumlilia akatangaze neno kwa nyimbo kwenye mimbari zao. Umetoweka.

Binadamu ufanyacho leo ni kwa ajili ya kesho yako. Ingawa hakuna ajuaye kesho. Ndo maana ya hujafa hujaumbika. Siku ukiwa peke yako umelala ardhini ukizungukwa na udongo pande zote. Ukizikwa ndiyo maana halisi ya ulivyoumbwa.

Mama wa watoto watatu. Muda mrefu alilalamikiwa kupokea pesa bila kutokea kwenye matamasha. Mwanzo ilionekana anachafuliwa na wanahabari.

Muda hauna urafiki na kiumbe chochote. Yametimia. Majaribu yanakuja wakati ambao viongozi wa dini hawako tayari tena. Kumtafuta, kumweka chini na kumlea kiroho. Kumtia moyo na ujasiri arudi kama awali. Kaachwa bila msaada.

Neno linasema ni yupi (mchungaji) ambaye akipoteza kondoo mmoja katika

mia anaowachunga, hatawaacha wale tisini na tisa mahali salama na kutoka kwenda kumtafuta mmoja aliyepotea? Wachungaji wa leo wanamuacha kondoo na dunia yake.

Wamekomaa na wale kondoo 99. Rose kaachwa. 

Ukristo unafundisha upendo ambao ulimvuta Rose kutoka imani nyingine na kujiunga nao. Pia tunaambiwa samehe unapokosewa. Kosa lake ni lipi lisilosameheka? Tumeamua kuhukumu?

Anaharibikiwa waimbaji wenzake wakimuangalia kama sinema. Ama pengine ni nafuu kwao kusikika. Ndo maana huoni wakifanya jambo kwa ajili yake. Anasemwa kwa mabaya tu. Tunaaminishwa hawezi kuwa mwadilifu tena.

Wiki hii imesambaa video ikionyesha anaombewa na mchungaji mmoja ambaye bila kutegemea akili ya CIA unagundua anatafuta ‘kiki’ tu. Rose kageuzwa kituko mpaka katika nyumba za ibada huku watu wanatazama kama Shilawadu. Inaumiza.

Haya mambo yapo kwa jamii yote. Thamani ya mtu ni pale anapokuwa na kitu. Mioyo yetu imejenga himaya ya roho chafu ya kutopenda kuona mwingine akifanikiwa. Kwenye tasnia ya muziki wa kidunia na kiroho ndo kambi rasmi ya ubinafsi na chuki. Hawapendani.
Via>>Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527