MBUNGE CCM AMTUHUMU WAZIRI WA UJENZI KUTOA KAULI YA KUMDHARAU WAZIRI MKUU

Mbunge wa Mafia, Mbaraka Dau (CCM), amemtuhumu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwele, akidai amekiuka agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, la kupeleka Mafia meli iliyotolewa na mfanyabiashara Said Salim Bakhressa akidai ni maagizo ya kisiasa.


Dau amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo Jumanne Novemba 6, wakati akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2019/20.


Alidai kuwa, suala la kupeleka meli hiyo Mafia walilijadili na Waziri Mkuu Majaliwa na akakubali ipelekwe Mafia jambo ambalo hata Profesa Makame Mbarawa aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, aliliridhia.


“Sasa hivi nimemfuata na kumkumbusha suala hilo lakini Waziri Kamwele anasema ni kauli za kisiasa, sasa inakuwaje waziri anasema agizo la Waziri Mkuu ni la kisiasa,” alihoji.


Alisema pia alimtuma mbunge mwenzake ili azungumze na Waziri Kamwele, lakini naye alijibiwa kuwa ili meli ipelekwe huko labda nauli iwe Sh 100,000.


Kabla ya mchangiaji wa mwisho kusimama, Waziri Kamwele alisimama na kusema; “Mbunge wa Mafia amenituhumu kuwa nilitoa maneno yanayoosha nimemdharau Waziri Mkuu, sijawahi kusema hayo maneno na waziri mkuu ila nakumbuka alinipigia simu akanimbia meli hiyo iliyotolewa na mfanyabiashara Bakhresa ifanye safari Mafia, nikatoa maagizo suala hilo liangaliwe kama linawezekana nikaambiwa meli hiyo inafanyiwa matengenezo,” amesema Kamwelwe akidai kauli ya Dau si nzuri kwa sababu Waziri Mkuu ni bosi wake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527