MAGARI 70 YA JWTZ YAPELEKWA MTWARA KUSOMBA KOROSHO

Magari 70 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWT) yameondoka jana Dar es Salaam kwenda mikoa ya kusini kuanza kazi ya kusomba korosho.

Mbali ya magari hayo, tayari askari kutoka Dar es Salaam na Kikosi cha 41 mkoani Mtwara wamepelekwa maeneo yote ambayo yanapaswa kulindwa kama Amiri Jeshi Mkuu, Rais Dk. John Magufuli alivyoagiza.


Akizungumza Dar es Salaam jana muda mfupi kabla ya msafara wa magari hayo kuondoka, Msemaji wa jeshi hilo, Meja Gaudence Ironda alisema taratibu zote zimekamilika baada ya kupokea maelekezo ya Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo.


“Magari zaidi ya 70 yameanza safari ya kwenda mikoa ya kusini kufanya ambayo tumeelekezwa na afande CDF (mkuu wa majeshi), haya ni maekelezo halali ambayo tunapaswa kuyatimiza,” alisema Meja Ironda.


Alisema magari hayo yatagawiwa katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ambako kuna kiasi kikubwa cha korosho ambazo zinapaswa kusombwa na kupelekwa katika maghala yanayohusika.


Meja Ironda alisema kazi hiyo itafanyika usiku na mchana kutokana na jeshi hilo kujipanga vizuri ili kuikamilisha kwa wakati.


“Kazi hii itafanyika usiku na mchana, tumepeleka askari wa kutosha ambao watalinda maeneo yote ambayo yanahusika na jukumu hili… nawaomba wananchi watulie, tunafanya hivi kwa mapenzi makubwa ya nchi yetu,” alisema.


Alisema Operesheni Korosho itajihusisha zaidi kutoa huduma ambazo wameelekezwa na si vinginevyo.


Naye Mkuu wa Kikosi cha Usafirishaji KJ 95 Mgulani, Luteni Kanali Elius Kejo alisema maandalizi yote yamekamilika na majukumu hayo yatatimizwa kama walivyoelekezwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post