MAMA AUA MTOTO WAKE KISA KAIBA MAEMBE ...AMTUNDIKA JUU YA MTI KUPOTEZA USHAHIDI

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia mwanamke mmoja aitwaye Rahel Matalaka (41), mkazi wa kijiji cha Lugenge, kwa tuhuma za kumpiga  fimbo hadi kumuua mtoto wake wa kiume Maliatabu Constantine (10) mwanafunza wa darasa la pili shule ya msingi Ikelege,wilayani Misungwi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, ACP Jonathan Shanna ,tukio hilo la mauaji limetokea Novemba,3 2018 majira ya saa moja usiku, baada ya mama wa marehemu kuletewa malalamiko kuwa mtoto wake alikuwa akiangusha na kuiba maembe kwa jirani.

 "Ndipo mtuhumiwa alipatwa na hasira na kumpiga mtoto kwa kutumia fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake hali iliyopelekea mtoto kupoteza fahamu na baadae kufariki dunia",

"Mtuhumiwa alipoona mtoto amepoteza maisha alimchukua na kumtundika juu ya mwembe kwa kutumia kipande cha khanga ili apoteze ushahidi ili baadae ionekane kuwa amejinyonga. Ndipo majirani walipoona tukio hilo walitoa taarifa kituo cha Polisi",alieleza Kamanda Shanna.

 Aidha alisema baada ya polisi kupata taarifa hizo walifanya ufuatiliaji wa haraka hadi eneo la tukio na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa.

Kamanda Shanna alisema jeshi la Polisi linaendelea na mahojiano na mtuhumiwa pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani na kwamba tayari mwili wa marehemu tayari umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527