DED MISUNGWI AYATAKA MASHIRIKA YANAYOJIHUSISHA NA UKIMWI KUJITATHMINI


Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Misungwi,mkoani Mwanza Kisena Mabuba ameyataka mashirika yanayojihusisha na mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kujitathmini wapi yamekwama kuzuia maambukizi ya VVU katika maeneo mbalimbali.

Alisema pamoja na kumekuwepo kwa utitiri wa mashirika na taasisi zinazojihusisha na masuala ya UKIMWI lakini maambukizi yanazidi kuongezeka.

Mabuba ametoa rai hiyo leo Jumanne Novemba 6,2018 wakati wa kikao cha wadau wa afya mkoani Mwanza kinachofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza.

“Mashirika ni mengi kwenye maeneo yetu, lakini maambukizi yamekuwa yakiongezeka,ni vyema mashirika haya pamoja na serikali yakajitathmini wapi yamekwama kuzuia maambukizi ya VVU kwani pesa nyingi na muda mwingi umekuwa ukitumika katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI lakini maambukizi yanazidi kujitokeza”,aliongeza.

Naye Katibu tawala wa mkoa wa Mwanza,Eng .Christopher Kadio amewataka wahusika wa mashirika na taasisi zinazotekeleza miradi ya afya kukutana na viongozi wa wilaya wanakotekeleza kazi wakiwemo wakuu wa wilaya ili waifahamu miradi hiyo na kutoa ushirikiano zaidi.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi mkoa wa Mwanza, Dk. Pius Masele Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) mkoani Mwanza yameongezeka na kufikia asilimia 7.2 kutoka asilimia 4.2 kuanzia mwaka 2012 hadi 2017.

Na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post