20 WAKAMATWA WAKILANGUA KOROSHO KWA WAKULIMA..YUMO DIWANI WA CUF

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homela.

Zaidi ya watu 20 wanaojihusisha kununua korosho kwa utaratibu usio rasmi kwa wakulima, maarufu kama kangomba wamekamatwa wilayani hapa akiwemo diwani wa Chama cha Wananchi (CUF).

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Juma Homera, alisema watu 14 tayari wamefikishwa mahakamani na wengine akiwemo diwani huyo wanaendelea kushikiliwa na polisi.

“Wananchi walitutumia sms (ujumbe mfupi wa simu) na tulitumia pia vyanzo vyetu vingine vilivyoko vijijini kubaini kangomba,” alisema Homera.

Alisema walimkamata mtu mmoja aliyekutwa akibadilishana na wakulima kwa kuwapa kilo moja ya nyama kwa kilo tatu za korosho.

“Huyo mtu alikutwa nyumbani katika Kijiji cha Nangorembe akiwa amechinja ng’ombe wanne, anagawa nyama kwa wananchi,” alisema.

Homera alisema pia katika Kijiji cha Kitanda walikamata watu saba waliokutwa na tani saba za korosho zenye thamani ya Sh milioni 75.

Alisema watu hao walikamatwa katika vijiji vya Mneche, Tinginya, Namiungo, Majimaji na Kitanda.

Kuhusu Diwani wa Kata ya Nalasi Magharibi, Khalifa Kabango (CUF), alisema alikamatwa juzi katika operesheni iliyofanywa Tarafa ya Nalasi ambako vilikamatwa viroba vya korosho 31 vikiwemo vya diwani huyo.

Alisema diwani huyo bado anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani Tunduru na kwamba alikuwa akinunua korosho kwa bei ya Sh 1,500 kwa kilo ili apeleke vyama vya msingi akapate fedha zaidi.

“Baadhi ya matajiri wamekuwa wakituma fedha vijijini na wenyeji ndio wanaonunua korosho hizo halafu wakikamatwa ndio wanawataja mabosi waliowatumia,” alisema.

Mkuu huyo wa wilaya alisema pia baadhi ya makarani wa vyama vya msingi wamekuwa wakitumia mawe ya mzani yaliyochezewa na kuwapunja wakulima.

Kwa mujibu wa DC huyo, mawe yaliyochezewa ni ya kilo 50 na kwamba katika kila jiwe la aina hiyo mkulima anaibiwa wastani wa kilo 5.5 hadi 6.

Alisema wamemkamata karani wa chama cha msingi, Mohamed Msamati kwa madai kuwa alikuwa akiwaibia wananchi kilo 5.5.

Kuhusu wakulima waliolipwa alisema hadi sasa wamelipwa 534 na Sh milioni 550.7 zimetumika.

“Tukimtilia mtu shaka kama kilo zake zimezidi tunakwenda kuangalia shamba lake kwanza halafu tunalinganisha na kilo alizopata mwaka jana,” alisema Homera.

Alisema hadi sasa zaidi ya tani 5,000 zimeshakusanywa katika maghala na zinaendelea kusafirishwa kupelekwa katika ghala kuu Mtwara kwa usimamizi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

“Hadi sasa tumeshasafirisha tani 166 na kilo 891 na magari matano ya JWTZ yameshaondoka na mengine matano yanaendelea kupakiwa,” alisema.

Homera alisema bado wanaendelea na kazi ya uhakiki wa majina ya wakuliwa wanaostahili kulipwa na kama kuna udanganyifu hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika.

Hata hivyo juzi wakati uhakiki wa majina ya wakulima wa korosho ukiendelea mkoani Mtwara, iliripotiwa kuibuka kwa majina hewa, likiwamo la mwenza wa karani wa chama cha msingi.

Katika uhakiki huo ambao unafanyika usiku na mchana kwa ajili ya malipo ya wakulima, yamebainika majina matatu katika Chama cha Msingi cha Makonga wilayani Newala.

Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Newala, Aziza Mangosongo, alisema walibaini majina hayo baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi.

Alisema mmoja wa makarani wa Makonga (jina linahifadhiwa), aliandika malipo hewa kwa jina la mpenzi wake (jina linahifadhiwa).

“Kutokana na uhusiano wao wa mapenzi, ameamua kumwandikia malipo hewa na kuna wengine wameandika ndugu zao.

“Tumekamata kilo 200 ambazo zimeandikwa malipo hewa, kama hali ndiyo hii kwa makarani wengine ikoje?

“Tunawaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano, wajumbe wa bodi, wenyeviti na makatibu wa Amcos zote wawe makini na waandike kile ambacho ni sahihi,” alisema Mangosongo.

Alisema karani huyo na wote waliohusika kuandika majina hewa wanaendelea kuhojiwa na utafanyika uhakiki katika kila shamba la mkulima na kujiridhisha na korosho alizowasilisha.

“Mtu hana shamba lakini unakuta jina lipo na akaunti namba, tukiwagundua wengine tutakula nao sahani moja,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post