KOROSHO ZA MAGENDO KUTOKA MSUMBIJI ZAKAMATWA TANZANIA

Zaidi ya tani tisa za korosho zimekamatwa zikiwa zimeingizwa nchini kwa njia ya magendo kutoka Msumbiji.

Tani hizo (magunia 91 ya kilo 100 kila moja) zilikamatwa juzi mpakani mwa Tanzania na Msumbiji eneo la Newala wakati wa operesheni iliyofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Newala, Aziza Mangosongo.

Wiki iliyopita, Rais Dk. John Mafuguli alitangaza kuwa Serikali itanunua korosho zote kwa bei ya Sh 3,300 kwa kilo na akatahadharisha vyombo vya ulinzi na usalama kuwa makini kuhakikisha hakuna zitakazoingizwa kutoka nchi jirani.

Akizungumza jana kwa niaba ya mkuu wa wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya ya Newala, Daniel Zenda, alisema Mtanzania mkazi wa Newala ndiye aliyekutwa na korosho hizo.

“Baada ya kuona rais ametangaza bei nzuri ya korosho, baadhi ya watu wameanza kutoa korosho za magendo kule (Msumbiji) kuja kuuza huku.

“Hizi korosho zilikutwa zikipimwa katika moja ya chama cha msingi kilichopo mpakani Masasi na huwa wanavusha kwa mtumbwi. Tulikamata pia trekta lililokuwa limezisomba,” alisema Zenda.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limewasili mkoani hapa na kuanza kukagua maghala ya kuhifadhia korosho wilayani Newala.

Wanajeshi hao walioongozana na Mangosongo, jana walikagua maghala matatu ambayo ni ya Micromix, Agro Focus na Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (Tanecu). Zenda alisema walipokea ujumbe wa wanajeshi 20.

Alisema pia viongozi wa vijiji, kata na vyama vya msingi wanaendelea kupewa maelekezo ya namna bora ya kufanya kazi hiyo kwa lengo la kuzuia uingizwaji wa korosho kutoka nchi jirani.

Ofisa Masoko wa Tanecu, Juma Selemani alisema kwa msimu wa mwaka 2018/2019 wanategemea kukusanya tani 120,000 na hadi kufikia jana walikuwa wamepokea zaidi ya tani 38,000 ambazo tayari zimeingia katika maghala makuu.

“Korosho zinaendelea kuletwa na taarifa za wakulima zimeshaandaliwa na kuwasilishwa sehemu husika kwa ajili ya malipo,” alisema Selemani.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa alipokea magari matano ya JWTZ ambayo yatakuwa na kazi ya kupunguza korosho kutoka maghala makuu kwenda katika maghala yatakayotumika kuzitunza kwa muda wakati zikisubiri kubanguliwa.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea maghala, viwanda vya kubangulia korosho pamoja na kupokea magari hayo, alisema mkoa unatarajiwa kupokea magari zaidi ya 75 kwa shughuli ya korosho zitakazoanza kubanguliwa hivi karibuni.

Byakanwa alisema bado nguvu ya wananchi wengine itatumika kama ilivyokuwa kawaida.

Alisema mkoa umesambaza timu ya watu watano kila wilaya kuhakiki majina na akaunti za wakulima.

Byakanwa alisema tayari uhakiki wa majina umeshakamilika na wakimaliza uhakiki wa akaunti malipo yatafanyika mara moja ili kuruhusu kazi ya ubanguaji kuanza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post