KANGI LUGOLA : MASHOGA WAPO SALAMA...SIJAPATA TAARIFA WAKILALAMIKIA USALAMA WAO

MBALI na ukweli kwamba Tanzania haiungi mkono watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja wakiwemo mashoga, imefafanuliwa kwamba maisha ya watu wa kundi hilo yako salama kama watu wengine hapa nchini.

Katika mahojiano na gazeti la Habarileo jana kuhusu madai kwamba wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja nchini maisha yao yako hatarini, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alifafanua wazi kwamba watu wa kundi kama hilo wapo salama.

“Ninachosema ni kuwa Tanzania ni salama na hakuna mtu yeyote anayeweza kusema kuwa sio salama bila ya kuwa na vigezo husika, kama mtu yeyote anahatarishiwa maisha yake, basi anapaswa kwenda Polisi na mimi sijapata taarifa zozote kutokea Polisi zinazoelezea kuwapo kwa mazingira hatarishi ya watu hao,” alisema.

Pia, alikanusha tetesi kuwa mashoga hao wamekuwa wakikimbia nchi na kuelekea nchi jirani, ikiwa ni sehemu ya kuomba hifadhi kutokana na kutokuwa na uhakika wa usalama wao.

Alisisitiza kuwa kwa upande wa mashoga, hajapata taarifa kutoka kituo chochote cha Polisi nchini, wakilalamikia usalama wao.

 Alisema kama kungekuwa na mazingira sio salama kwao, wangeenda kupeleka malalamiko yao kwenye vituo vya Polisi jirani; na kuwa akiwa waziri mwenye dhamana, hajapata taarifa za mazingira hatarishi kwa mashoga nchini.

Hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliwataka wananchi kumtajia majina ya mashoga wa Dar es Salaam, kwa njia ya simu yake ya mkononi.

 Kutokana na agizo hilo, watu kadhaa wamekuwa wakiendelea kumtajia majina hayo, hali ambayo imesababisha taharuki kwa baadhi ya watu waliotajwa, huku wengine wakilalamikia utaratibu huo, hasa mashirika ya haki za binadamu yakiwamo ya nje ya nchi.

Tangu jana kuna video fupi ya mahojiano kati ya Shirika la Utangazaji la Marekani, RTE News na Mwanaharakati ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Haki za Binadamu, Frontline Defender, Erin Kilbride akizungumzia agizo hilo la Makonda, akidai kuwa amepata taarifa kuwa mashoga wanalalamikia usalama wao.

Mkurugenzi huyo alisema mashoga hao, wamekuwa wakihatarishiwa maisha yao na wananchi kutokana na harakati hizo za mkuu wa mkoa za kutaka majina yao yatajwe na kutoa tamko kuwa anataka kuumaliza ushoga.

Via Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527