Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya Ivory Coast, Didier Drogba ameweka wazi kuwa aliwahi kuzuiliwa kucheza mpira kwa mwaka mmoja na baba yake mzazi, mzee Albert Drogba ili ajikite zaidi kwenye elimu.
Drogba ambaye amestaafu kucheza soka, ameeleza kuwa akiwa na miaka 16 baba yake alimwambia aachane na mpira kwani hauna faida kama ambavyo atajikita zaidi kwenye elimu ambayo itamsaidia katika maisha yake ya baadae hivyo ilimlazimu kutocheza soka kwa mwaka mmoja.
"Baba yangu aliniambia mpira hapana, si kazi salama inaweza kukujeruhi na ukapoteza kila kitu hivyo sikucheza tena kwa mwaka mmoja, lakini ilikuwa shauku yangu na kazi ninayoipenda ambayo ni wazi sasa imenipa pesa nyingi na nimewekeza mpaka kwenye elimu'', amesema.
Drogba ameendelea kwa kusema kuwa baada ya baba yake kuona kijana wake hana raha, alimkubalia acheze mpira jambo ambalo anaamini limeisaidia jamii kubwa na pengine kila mzazi anafurahia akiona mtoto wake anacheza soka.
Drogba amestaafu soka akiwa amecheza mechi 497 ngazi ya klabu na kufunga mabao 210. Kwa upande wa timu ya taifa ya Ivory Coast ambayo ameichezea tangu mwaka 2002 hadi 2014, amecheza mechi 104 na kufunga mabao 65.
Chanzo:-Eatv