DC Katambi Atangaza Fursa Kubwa Kwa Wafanyabiashara Na Wakulima



Charles James

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobas Katambi amewataka wafanyabiashara nchini kuchangamkia fursa zilizopo jijini humo ili kuunga mkono juhudi za kimaendeleo zinazofanywa na Rais John Magufuli katika kuhakikisha Tanzania inakua Nchi ya Viwanda.

Akizungumza na wanahabari mara baada ya kumalizika kwa tamasha la zabibu lililozinduliwa kwenye viwanja vya Mashujaa jijini humo na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, DC Katambi amewataka wawekezaji wakiwemo wafanyabishara na wakulima kuchangamkia fursa ya kuwekeza kwenye zabibu kwani muda ndio sasa.

Amesema ni jambo la faraja kuona sasa zao la Zabibu linatangazwa kimataifa na kuzinduliwa kwa tamasha hilo na Mama Samia kutalifanya zao hilo kuzidi kupewa kipaumbele sawa na mazao mengine kama Mchikichi, Korosho na hivyo kuwa zao kubwa la kibiashara ndani na nje ya Nchi.

“ Ni zao linalotoa matunda mengi na linazalisha bidhaa nyingi sana, kwa mfano unaweza kupata mchuzi wa zabibu, vile vile unapata dawa, zabibu ni tunda unaweza kutengeneza juisi lakini pia inazalisha kilevi(pombe),” amesema Katambi.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kwa sasa kipaumbele chao kama wananchi wa Dodoma ni kuhakikisha wanatafuta masoko mengi,kutafuta viwanda kwa ajili ya kuchakata zabibu lakini pia kulikuza zao hilo ili kulizidishia thamani ili kuweza kuwapa faida wakulima.

“ Wafanyabiashara waje kuwekeza Dodoma nawakaribisha sana hii ni fursa kwao kutengeneza vipato vyao na kukuza uchumi wetu kwa sababu zabibu inakupa fursa kubwa kama ambavyo nimeeleza kazi zake hapo awali, kwa sasa tunafanya master plan kuangalia maeneo ya pembeni yatakayokua mashamba, kuhamasisha kika mwanafamilia mmoja kuwa na shamba la zabibu,’ amesema DC Katambi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527