CCM YAFUNGA RASMI PAZIA LA KUWAPOKEA WABUNGE NA MADIWANI KUTOKA UPINZANI

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza rasmi kufunga pazia la kuwapokea viongozi, wabunge na madiwani wanaohamia chama hicho kutoka upinzani.

Akitangaza kufungwa kwa suala hilo jana mjini Morogoro, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, alisema leo ndio mwisho wa kupokea viongozi, madiwani na wabunge kutoka vyama vya upinzani na kwamba atakayetaka kujiunga na chama hicho baada ya hapo atakuwa mwanachama wa kawaida.

“Huu ni uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM kwamba ifikapo Novemba 15 iwe mwisho wa kupokea viongozi, madiwani na wabunge kutoka upinzani, hivyo leo nimefunga rasmi jambo hili. Baada ya hapo, atakayetaka kurudi atabaki kuwa mwanachama wa kawaida,” alisema.


Wakati akitangaza hilo jana, tangu kuanza kwa hamahama ya wabunge na madiwani wa upinzani, CCM imeshapokea zaidi ya wabunge na madiwani 150 ambao pamoja na kujiengua upinzani, waliteuliwa na CCM kugombea nafasi zao na kushinda.


Wabunge waliojiuzulu nyadhifa zao kutoka upinzani ni Pauline Gekul (Babati Mjini), Mwita Waitara (Ukonga), Joseph Mkundi (Ukerewe), James ole Millya (Simanjiro), Dk. Godwin Mollel (Siha), Julius Kalanga (Monduli) na Chacha Ryoba (Serengeti) wote kutoka Chadema, Zuberi Kachauka na Maulid Mtulia (kutoka CUF).


Mbali na wabunge hao, wengine ambao walijiengua upinzani ni pamoja Anna Mghwira, aliyekuwa mgombea urais kupitia ACT-Wazalendo ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.


Wengine ni Profesa Kitilla Mkumbo ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, David Kafulila, Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patroba Katambi, sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma.


Viongozi hao, wakiwamo wabunge, wakati wa kutangaza uamuzi wao wa kujiunga na CCM walisema wamefanya hivyo, ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya Rais John Magufuli katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527