AGAPE YAENDESHA KIKAO CHA KUTOKOMEZA NDOA NA MIMBA ZA UTOTONI KATA YA USANDA - SHINYANGA


Shirika lisilo la serikali la Agape mkoani Shinyanga limeendesha kikao na viongozi wa kata ya Usanda halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakiwemo wa kidini,kimila,wazazi,walimu pamoja na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili kujadili  mikakati ya kutokomeza ndoa na mimba za utotoni. 

Akizungumza leo Novemba 15,2018 wakati wa ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika katika shule ya msingi Usanda Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Agape John Myola alisema kikao hicho ni kwa ajili ya kujadili vikwazo vinavyojitokeza kwenye mapambano ya kutokomeza ukatili wa kijinsia ikiwemo matukio ya ndoa na mimba za mapema ambapo mkoa wa Shinyanga unatajwa kuwa na kiwango cha juu cha ndoa za utotoni. 

“Tumekutana hapa kuona namna gani kwa ushirikiano wetu tunaweza tukaukomboa mkoa wetu na vitendo hivi vinavyokatisha ndoto za watoto wetu,kwa mujibu wa utafiti wa shirika la watoto duniani UNICEF mwaka 2017 zimeutaja mkoa wa Shinyanga kuwa na asilimia 59 ya ndoa za utotoni,huku vitendo vya ukatili ikiwa ni asilimia 78” ,alisema myola. 


Meneja Mradi wa Afya ya Uzazi na Ujinsia mradi unaotekelezwa kata ya Usanda kwa ufadhili wa shirika la SIDA Sweden na kutekelezwa na shirika la AGAPE Lucy Maganga, alisema wameanza kuyafikia maeneo ambayo yalikuwa ni vigumu kufikika kutokana na ubovu wa miundombinu ili kutoa elimu hiyo na kulinusuru kundi la watoto wa umri wa miaka 10-15. 


“Tuna lengo la kuwafikia watoto 1500 kati yao wa kike 800 na kiume 700 katika maeneo ya Munge,Uswahilini,Mwagala,Buchamiki na Sagabahi” ,alisema.

Kaimu Afisa Maendeleo ya jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Edmund Ardon aliwataka wananchi kwa nafasi zao kuwa mstari wa mbele kupinga ndoa na mimba za utotoni. 

“Ndugu zangu elimu kuhusu masuala ya haki imezidi kuenea katika maeneo tofauti katika halmashauri yetu,tunapaswa kila mmoja asimame kukemea vitendo hivi anapopata taarifa ama kuvishuhudia ili tuwe mfano wa kuigwa na halmashauri zingine,” alisema Ardon. 

Aidha washiriki wa kikao hicho walieleza kusikitishwa na vitendo vya  baadhi ya ya wazazi,sheria na vyombo vya maamuzi kushindwa kutoa ushirikiano kwenye kesi za ndoa na mimba za utotoni.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia Lucy Maganga akizungumza wakati wa kikao cha kujadili namna ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni katika kata ya Usanda halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Agape John Myola akizungumza wakati wa kikao cha kujadili namna ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni katika kata ya Usanda.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Agape John Myola akiwataka wadau wote kuungana kupambana na ndoa na mimba za utotoni.
Afisa Mtendaji Kata ya Usanda Maduhu Emmanuel akieleza namna wanavyokabiliana na tatizo la mimba na ndoa za mapema katika kata ya Usanda.
John Komba mwakilishi wa shirika la Sida akizungumza wakati wa kikao hicho.
Mchungaji Lameck Makungu kanisa la AICT Usanda akichangia hoja wakati wa kikao hicho.
Wanafunzi wakiandika dondoo muhimu wakati kikao hicho.
Washiriki wa kikao hicho wakiendelea na majadiliano.
Mwanafunzi wa shule ya Sekondari Samuye Emmanuel Jonas akichangia hoja wakati wa kikao hicho.
Mwalimu wa shule ya msingi Busanda Clads Gwamagobe akizungumza wakati wa kikao hicho.
Mmoja wa washiriki wa kikao hicho akichangia hoja.
Mzazi akichangia mada wakati wa kikao hicho.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Singita akichangia hoja wakati wa kikao hicho.
Viongozi wa kidini na kimila wakati wa kikao.
Kaimu Afisa Maendeleo ya jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Edmund Ardon akiwasilisha maazimio ya kikao hicho.
Picha ya pamoja washiriki wa kikao cha kuweka mikakati ya kutokomeza ndoa na mimba za mapema.


Picha zote na Malaki Philipo – Malunde1 blog.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post