BOSI WA MABASI YA MWENDO KASI ANUSURIKA KUFUKUZWA KAZI...JPM AMFYEKELEA MBALI KISHA KUMSUKUMA NDANI TENA


 Rais John Magufuli ametengua nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Mabasi ya Mwendokasi (Dart), Ronald Lwakatale na kumteua Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) Mkoa wa Singida, Leonard Kapongo lakini dakika 10 baadae akabatilisha uamuzi huo.

Hali hiyo ilijitokeza leo wakati Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alipowaambia waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu kutenguliwa kwa mkurugenzi huyo.

Alisema hata hivyo hivi karibuni kumekuwa na mdororo mkubwa na kwamba jambo hilo haliridhishi kabisa.

“Jambo hili katika ofisi yangu halitutiii amani kabisa. Kutokana na hilo Mheshimiwa Rais ambaye ni mwenye dhamana tawala za mikoa na Serikali za mitaa ameridhia kutenguliwa kwa mtendaji mkuu wa wakala huo Mhandisi Ronald Lwakatare na yeye atapangiwa kazi nyingine.” .

“Nafasi yake itachukuliwa na Mhandisi Leonard Kapongo ambaye ni Meneja wa Tanroad Mkoa wa Singida na uteuzi huo unaanza leo mara moja. Jukumu lake kubwa sasa atakwenda kuweka utaratibu mzuri wa kurudisha hali nzuri ya usafiri katika jiji la Dar es Salaam.”

Baada ya kumalizika kwa mkutano huo, waandishi waliondoka na walipofika getini walielezwa na walinzi kwamba wanaitwa tena na Waziri Jafo.

Mara baada ya kurejea, Jafo alizungumza tena na waandishi akisema kuna mabadiliko kuhusu taarifa hiyo kwamba mkurugenzi huyo aliyetumbuliwa ataendelea na shughuli zake kama kawaida ila anatakiwa kujitathimini.

“Na leo hii kama mmeshuhudia kuwa watu wengine wamepita katika madirisha na nikiwa kama Waziri wa Tamisemi siridhiki na mwenendo huu namuagiza mtendaji mkuu anipe taarifa nini kinachoendelea. Kwa nini kuna hali ya kusuasua?” alisema.

Na Sharon Sauwa, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527