WAZIRI KUU KASSIM MAJALIWA ASIFU UTENDAJI WA TARURA

Na Yusuph Mussa, Bahi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini nchini (TARURA) ameleta ukombozi mpya katika kushughulikia kero za muda mrefu za ubovu wa barabara, kwani tangu wameanza takribani miaka miwili iliyopita wameonesha jitihada za dhati kukabiliana na changamoto hiyo.

Akizungumza leo Oktoba 19, 2018 kwenye uzinduzi wa Daraja la Chipanga, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea wilaya za mkoa wa Dodoma, Majaliwa alisema Serikali haikufanya makosa kuanzisha TARURA, kwani kwa muda mfupi wameanza kuona mafanikio yake nchi nzima.

Akimtambulisha Mkurugenzi Mtendaji wa TARURA nchini Mhandisi Abdul Digaga mbele ya wananchi wa Chipanga, Majaliwa alisema kujengwa kwa daraja hilo kumewaondolea adha wananchi wa upande wa pili ambao wakati wa mvua nyingi walikuwa wanashindwa kwenda Makao Makuu ya Wilaya hiyo mjini Bahi.

"Niwapongeze TARURA wamefanyakazi nzuri tangu kuanza kwake, na sio daraja hili tu, bali wamefanikisha kutengeneza barabara nyingi na madaraja karibu nchi nzima. Na daraja hili nalifahamu ilikuwa ni kero kwa wananchi kuweza kuvuka hapa kwenda Makao Makuu ya Wilaya, Bahi" ,alisema Majaliwa.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Suleiman Jafo alisema mradi huo wa Daraja la Chipanga linalounganisha baadhi ya vijiji ikiwemo Chigongwe na Chipanga, ujenzi wake ulianza Oktoba 3, 2016 na kukamilika Mei, mwaka huu kwa gharama ya sh. bilioni 2.1.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Rachel Chuwa alisema, pamoja na vijiji vya Chigongwe na Chipanga kunufaika kwa daraja hilo, pia litasaidia vijiji vya Chimpelo, Chali Makulu, Chali Igongo na Chali Isanga.

"Kukamilika kwa daraja hili ni muhimu sana kwa wananchi, kwani wakati wa msimu wamvua walikuwa wanashindwa kufanya shughuli zao kwa vile mawasiliano yanakatika, lakini kwa sasa daraja hili halinufaishi vijiji vya Wilaya ya Bahi tu, bali hata wananchi wanaotoka Wilaya ya Dodoma kwenda Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, hiyo ni njia ya mkato", alisema Chuwa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa tatu kushoto) akiweka jiwe la msingi la ufunguzi wa Daraja la Chipanga, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma leo Oktoba 19, 2018. Wengine ni Waziri wa TAMISEMI Suleiman Jafo (kushoto), Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma George Mkanwa (wa pili kulia), Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi Mukunda (wa tatu kulia), Mbunge wa Jimbo la Bahi Omar Baduel (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Rachel Chuwa (kulia). (Picha na Yusuph Mussa).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi la ufunguzi wa Daraja la Chipanga, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma leo Oktoba 19, 2018.
Muonekano wa Daraja la Chipanga, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma ambalo limefunguliwa leo Oktoba 19, 2018 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post