SERIKALI YAZINDUA MFUMO WA UBORESHAJI UPATIKANAJI DAWA


 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI),Selemani Jafo akizungumza  na wadau mbalimbali wa afya katika  hafla ya uzinduzi wa mfumo wa mshitiri Kitaifa leo jiji Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka wa Global ya jamii)
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI),Selemani Jafo akizindua mfumo wa kitaifa wa uboreshaji upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kupitia mshitiri (Mzabuni binafsi) jana jijini Dar es Salaam.(kushoto) Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,Paul Makonda.(Picha na Emmanuel Massaka wa Global ya jamii). 
 Sehemu ya wadau wa afya wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa mfumo wa Mshitiri Kitaifa jana jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja

Na Said Mwishehe,

SERIKALI imezindua mfumo wa kitaifa wa uboreshaji upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kupitia mshitiri(Mzabuni binafsi).

Mfumo huo maarufu kwa jina la Jazia unalenga kuongeza ufanisi wa upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vinavyokosekena Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya katika vituo vya tiba.

Mfumo huo umezinduliwa rasmi leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ofisi ya Rais(TAMISEMI) Suleiman Jaffo ambapo amesema unakwenda kusaidia kuondoa changamoto ya kukosekana kwa dawa na vifaa tiba katika vituo vya tiba.

"Mfumo huu wa uboreshaji upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kupitia mshitiri kutaongeza kasi ya upatikanaji dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara ili kupunguza muda wa kusubiri huduma na kupatikana kwa bidhaa za afya wakati wote,"amesema Jaffo.

Ameongeza mfumo huo ambao umezinduliwa rasmi leo utakuwa ni wa nchi nzima na kutoa maagizo kwa mikoa yote nchini kujiunga na mfumo huo na ifikapo Oktoba 30 mwaka huu na tayari unatumika nchini kote.Amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi madhubuti wa Rais Dk.John Magufuli moja ya vipaumbele vyake ni kuboresha sekta ya afya nchini kwa kuondoa changamoto zilizipo.

"Hivyo mfumo huu unakwenda kumaliza tatizo la kukosekana kwa dawa katika vituo vya tiba,"amesisitiza.Amesema anatambua na kuthamini kazi nzuri ya MSD katika kusambaza dawa na vifaa tiba lakini mfumo huo utasaidia pale ambapo MSD wameshindwa kufikisha dawa au vitaa tiba hivyo.Ametoa maagizo kwa halmashauri zote nchini kuanzia sasa baada ya mfumo huo kuzinduliwa rasmi upatikanaji wa dawa katika vituo vya tiba uwe asilimia 98 na kuwataka wakurugenzi wa halmashauri kushiriki kikamilifu.

Amesisitiza ni matumaini yake mfumo huo umekuja kumaliza tatizo la kukosekana kwa dawa na kama tatizo basi limepata tiba yake.Kikubwa ni kuhakikisha mfumo unasimamiwa vema kwa maslahi ya Watanzania wote.Ametumia nafasi hiyo kuzungumzia mikakati ya Serikali ya Awamu ya tano katika kuboresha sekta ya afya ikiwemo ya ujenzi wa hospitali za Wilaya na ujenzi wa vituo vya afya na lengo ni kuu ni kuboresha sekta ya afya nchini.

Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Grace Magembe amesema mfumo huo ambao umezinduliwa leo wao waliamua kuufanyia utafiti na kubaini utamaliza tatizo la kukosekana kwa dawa na vifaa tiba ndani ya mkoa huo."Kwetu sisi ni tofauti na mikoa mingine tuliamua kufanya utafiti kwanza na kubaini mahitaji halisi ya dawa na vifaa tiba.Hivyo leo tunaingia mkataba na wazabuni wetu tukijua mahitaji yetu,"amesema .

Amefafanua wakati wa utafiti huo wamebaini mambo mengi kwani wamegundua kuna kampuni ambayo kazi yake ni vifaa vya umeme lakini ilipewa jukumu la kusambaza dawa.Amesema hivyo kupitia mfumo huo ambao umezinduliwa wapo makini kwa kuhakikisha wanaopewa jukumu la kusambaza dawa na vifaa tiba wamekidhi vigezo vyote na watalaam wa kada mbalimbali wameridhika.Amesema kwa Mkoa wa Dar es Salaam mzabuni binafsi ambaye amepewa jukumu hilo ni Bahari na Umoja ambao wameingia nao mkataba na kikubwa zaidi bei ambayo itatumika ni ile ambayo ipo sawa na bei ya MSD au chini.

Kuhusu mfumo huo imeelezwa umejaribiwa kwa miaka minne katika mikoa ya Dodoma,Morogoro na Shinyanga tangu mwaka 2014.Mpango huo ulianzishwa na mradi wa ushirikiano wa nchi mbili kati ya Tanzania na Uswisi kupitia mradi wa Health Promotion and System Strengthening (HPSS) ambao pia unajulikana kama "Tuimarishe Afya Proejct" unaofadhiliwa na na Serikali ya Uswi
si.

Pia kwa muda mrefu usambazaji wa dawa na vifaa tiba nchini umekuwa ukifanywa na sekta ya umma pekee kupitia MSD lakini pamoja na juhudi zote za MSD kutokana na ukubwa a nchi wamekuwa wakisambaza dawa na vifaa tiba kati ya asilimia 50 hadi asilimia 60.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post