SERIKALI KUFUNGA CCTV CAMERA KATIKA MAJIJI YOTE NCHINI ILI KUKABILIANA NA MATUKIO YA UTEKAJI

Serikali inatarajia kusambaza kamera maalum za CCTV katika miji mikubwa na mikoa iliyoko karibu na mipaka ya nchi kwa lengo la kuimarisha ulinzi, na kukomesha matukio ya kihalifu ikiwemo matukio ya utekaji.


Hayo yamesemwa jana Oktoba 14, 2018 jijini Arusha na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kwenye ziara ya kutembelea vitengo vya wizara yake vilivyoko jijini humo, ambapo amesema mazingira ya utendaji kazi wa polisi yamekuwa na changamoto nyingi ambazo baadhi yake zinakwaza utekelezaji wa majukumu yao hivyo Serikali imeamua kuwaongeza nguvu ili kurahisisha majukumu yao.


“Tunampango wakufunga CCTV Camera hasa katika miji mikuu ili kupunguza matukio mbalimbali ikiwemo suala la utekaji, hata ukiangusha sindano lazima ionekane, na ninawaonya wanasiasa uchwara wasitumie tukio hili kujipatia umaarufu”, amesema Masauni.


Masauni ameongeza kuwa , “Matukio ya utekaji ni sifa mbaya sana ila sitaki kulielezea sana maana jana (juzi) Waziri wa Mambo ya Ndani amezungumza mengi ikiwemo mafanikio ya jeshi la polisi, ila hili la mfanyabiashara Mohamed Dewji limechukua sura kubwa hadi duniani kutokana na umaarufu wake na linatisha hata watalii lakini niseme serikali ina mikakati ya kutokomeza hili”.


Taarifa za kutekwa kwa mfanyabiashara huyo anayekadiriwa kuwa na utajiri wa Sh3.5 trilioni zilianza kusambaa Alhamisi ya Oktoba 11, saa 1:00 asubuhi katika mitandao ya kijamii, kabla ya polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam kuthibitisha saa mbili asubuhi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post