MWALIMU MBARONI KWA TUHUMA YA KUMLAWITI MWANAFUNZI WA DARASA LA TANO

Na John Walter-Babati
Jeshi la polisi mkoa wa Manyara linamshikilia Mwalimu wa shule ya Msingi Rift Valley English Medium mkazi wa mruki mjini Babati kwa tuhuma za kumlawiti Mwanafunzi wake wa kiume [11] anayesoma darasa la tano.

Kaimu Mganga mfawidhi wa Hospitali ya mji wa Babati Mrara Dr. Catherine Palanjo amethibitisha kupokelewa kwa mtoto huyo [jina tunalihifadhi],ambaye aliambatana na mzazi wake [mama] mkazi wa Angoni pamoja na askari polisi ambapo walipatiwa huduma na vipimo vyote vilivyohitajika na daktari wa zamu na baada ya hapo akarudi nyumbani.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara Agustino Senga amesema limetokea Septemba 28.2018 majira ya saa saba mchana ambapo Mama wa mtoto aliefanyiwa ukatili huo Silivia William[42] daktari wa kituo cha afya Galapo Mkazi wa Angoni C aligundua kuwa mwanae hayupo katika hali ya kawaida ndipo alipomuhoji na kumjibu kuwa amefanyiwa kitendo cha ulawiti na mwalimu wake ajulikanaye kwa jina la Charles Melkiory maarufu Msele [32] mkazi wa mtaa wa Mruki kata ya Maisaka wakati wakiwa wanaendelea na vipindi vya dini shuleni hapo.

Kamanda ameeleza kuwa siku ya tukio mwanafunzi huyo alikuwepo shuleni ambapo ilipofika mapumziko ya kunywa uji saa 4:00 asubuhi mwanafunzi mwenzake wa darasa la tano alimfuata na kumueleza kuwa mwalimu [mtuhumiwa] anamuhitaji ofisini kuna maelekezo anataka kumpatia, na alipofika alimwambia urudi saa tano,lakini ilipofika muda wa kipindi cha dini alimwambia kwamba tutakutana bwenini kuna jambo la msingi nataka kukuambia.

Kamanda aliendelea kwa kueleza kuwa ilipofika majira ya saa saba mchana mwanafunzi huyo akiwa na mwenzake ambaye yupo bweni alikwenda kuchukua daftari na kwenda wote,yule wa bweni akarudi darasani kwenye kipindi cha dini lakini yeye alibaki kusubiri maelekezo ya mwalimu wake ambaye alifika na kumvua nguo na kumuingilia kwa kumpaka mafuta huku akimpa vitisho vikali na kwamba asimweleze mtu yeyote.

Akizungumza mkuu wa shule ya Rift Valley Babati kwa upande wa Sekondari Dadly Wilfredy amesema tukio hilo ni la mara ya kwanza kutokea na kwamba sio desturi ya shule hiyo na kuwataka wazazi wenye wasiwe na hofu kwani walimu wapo kwa ajili ya kuwasaidia watoto ambapo kwa sasa wamejipanga kuwapa ushauri na ulinzi madhubuti.

“Huyu mwalimu kwanza ni mgeni sana hapa shuleni hana hata mwaka,amepata hii ajira ndani ya miezi sita tu,kwa hiyo hatujaweza kutambua kikamilifu tabia yake ila tunavyojua ni kwamba kwa walimu waliopo shuleni zaidi ya miaka sita hatujawahi kumona yeyote mwenye tabia mbaya,hawa watu wanaweza kusema hivyo kwa Interest zao lakini msema ukweli ni pale upelelezi utapofika mwisho na kuweza kutoa taarifa kamili,”alisema Mwalimu Wilfredy.

Kwa upande wa afisa Maendeleo ya Jamii mji wa Babati Jackline Gudluck ametoa ushauri kwa wazazi kuhakikisha kuwa wanakuwa karibu na watoto wao na kuzungumza nao na sio kuwakemea ili waweze kugundua changamoto mbalimbali zinazowakabili pindi wanapokuwa mashuleni.

Jeshi la polisi mkoa wa Manyara limeeleza kuwa linamalizia upelelezi wa tuhuma hizo na mtuhimwa yupo mahabusu na muda wowote atafikishwa mahakamani kujieleza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527