WANAFUNZI 25,532 WAPANGIWA MIKOPO MWAKA WA MASOMO 2018/19..ORODHA AWAMU YA KWANZA IMETOKA


BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inapenda kuwafahamisha waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/2019 kuwa imetoa orodha ya Awamu ya Kwanza yenye jumla ya waombaji wa mwaka wa kwanza 25,532 waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 88.36 bilioni.

Akitangaza orodha hiyo leo (Jumatano, Oktoba 17, 2018) jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru amesema kati ya wanafunzi hao, wanaume ni 16,085 na wanawake ni 9,447.

Bw. Badru ameongeza kuwa katika awamu hiyo ya kwanza HESLB pia imetoa mikopo yenye thamani ya TZS 850.35 milioni kwa watanzania wanafunzi 69 wanaoendelea na masomo nje ya nchi chini ya makubaliano maalum na nchi rafiki zipatazo saba ambazo ni Msumbiji, Algeria, Cuba, Urusi, Serbia, Urusi na Ujerumani.

Bajeti ya TZS 427.5 bilioni zimetengwa kwa mikopo ya elimu ya juu 2018/2019
Katika mkutano huo, Bw. Badru ameeleza kuwa bajeti ya fedha za mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2018/2019 ni TZS 427.5 bilioni na tayari Serikali imeshatoa TZS 137.06 bilioni zinazohitajika wakati vyuo vinafunguliwa mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba na mwezi Novemba (2018). Kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo wapatao 123,285.

“Fedha nyingine tutazipokea baadaye katika robo ya pili ya mwaka wa fedha kwa ajili ya malipo ya wanafunzi watakaopangiwa mikopo … kwa hiyo kwa sasa, tuna fedha tunazohitaji kwa waombaji wote wenye sifa,” amesema Bw. Badru katika mkutano uliohudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Uchambuzi na Upangaji Mikopo wa HESLB Dkt. Veronica Nyahende.

Kuhusu kutangaza Awamu ya Pili
Bw. Badru amesema kuwa HESLB itaendelea kutoa awamu nyingine za orodha za wanaopangiwa mikopo kadri itakavyokamilisha uchambuzi wa orodha za wanafunzi walioomba mikopo na ambao pia wamepata na kuthibitisha udahili wao katika chuo kimoja ili kuhakikisha fedha za mikopo zinawafikia wanafunzi wahitaji katika vyuo walivyothibitisha.

Upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa pili na kuendelea
Aidha, Bw. Badru amesema kuwa wanafunzi wenye mikopo na wanaoendelea na masomo wataendelea kupata mikopo ikiwa wamefaulu mitihani yao na matokeo yao kuwasilishwa HESLB na vyuo husika.

“Tunatoa mikopo ili mwanafunzi asome, kwa hiyo tutaendelea kuwapa mikopo wanafunzi wenye mikopo na wanaendelea na masomo ikiwa tumepokea uthibitisho kuwa ana sifa za kuendelea na masomo katika mwaka unaoanza hivi punde,” amesema Bw. Badru.

Upatikanaji wa orodha kamili ya waliopangiwa mikopo
Majina yote ya waombaji waliofanikiwa kupangiwa mikopo katika awamu hii ya kwanza yataanza kupatikana baadae leo katika mtandao wa HESLB wa uombaji mkopo (https://olas.heslb.go.tz) na tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz). Aidha, orodha ya majina hayo pia zinatumwa vyuoni kwa ajili ya kurahisisha taratibu za usajili wa wanafunzi hao.

Lengo la Bodi ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wenye sifa ya kupata mikopo katika mwaka wa masomo 2018/2019, wanapangiwa mikopo kabla vyuo kufunguliwa mwishoni mwa mwezi Oktoba, mwaka huu (2018).

Aidha, Bodi inapenda kuwasihi waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati mchakato wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kwa awamu inayofuata ukiendelea.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano,
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Jumatano, Oktoba 17, 2018

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post