MAGUFULI : SERIKALI ITAENDELEA KUMUENZI BABA WA TAIFA

Rais John Magufuli amesema Serikali itaendelea kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuhakikisha fikra na mipango mizuri aliyoiweka inatekelezwa kwa manufaa ya Watanzania wote.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Oktoba 14, 2018 wakati akizungumza na mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere nyumbani kwake Msasani Jijini Dar es Salaam alikokwenda kumtembelea muda mfupi baada ya kushiriki Misa Takatifu iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay.

Taarifa iliyotolewa leo na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imemnukuu Rais Magufuli akisema Mwalimu Nyerere alifanya kazi kubwa ya kujenga misingi imara ya nchi kuwa na amani, umoja na mshikamano na pia kujenga misingi ya uchumi wa kujitegemea kupitia Azimio la Arusha.

Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania wote hasa vijana kuungana na Serikali katika kuyaenzi yaliyofanywa na Baba wa Taifa na pia kuliombea Taifa.

Naye Mama Maria Nyerere amemshukuru Rais Magufuli kwa kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa na amemhakikishia yeye na wana maombi wenzake pamoja na Watanzania wote wanamuombea heri yeye, viongozi wote na Taifa kwa ujumla.

Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth amekutana na mtoto wa Baba wa Taifa, Makongoro Nyerere na wajukuu wa Baba wa Taifa.

Waumini hao kwa pamoja wamemuombea Baba wa Taifa, aliyefariki dunia Oktoba, 14 1999 ambako katika mahubiri yake, Paroko Msaidizi Padre Barthlomeo Bachoo amesema katika uhai wake Hayati Baba wa Taifa aliongoza Taifa kwa hekima kubwa, alipenda amani, haki, alipiga vita ukoloni, udini, ukabila, rushwa, uonevu na alikuwa mcha Mungu aliyekuwa akisali katika kanisa hilo.

“Tunapomkumbuka Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere kila Mtanzania ana wajibu wa kuliombea Taifa, kuwa balozi wa amani, upendo, umoja na mshikamano na pia tuwaombee viongozi wetu waishi falsafa ya Mwalimu Nyerere, tusimtafute Mwalimu Nyerere makaburini bali tumtafute katika mambo aliyotufundisha” amesema Padre Bachoo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post