RAIS MAGUFULI AWAPA PRESHA WAKUU WA MIKOA NA WILAYA ..ATAKA WAJIELEZE


Rais John Magufuli ameagiza wakuu wa mikoa na wilaya katika halmashauri tano nchini zilizofanya udanganyifu kwa miradi iliyotembelewa na Mwenge wa Uhuru mwaka jana, wajieleze kabla ya kuchukuliwa hatua.

Pia, Rais Magufuli amewataka wakuu wa mikoa na wa wilaya zote ambazo zimekutwa na miradi yenye dosari kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kutoa maelezo ndani ya siku 10 na kurekebisha dosari zilizojitokeza.

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo jana alipokutana na kufanya mazungumzo na wakimbiza Mwenge wa Uhuru mwaka huu waliomtembelea Ikulu jijini Dar es Salaam na kuwapongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Waziri Mkuu kutoa siku 10 kwa halmashauri 64 ambazo Mwenge wa Uhuru ulishindwa kuzindua au kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya maendeleo iliyokutwa na dosari.

Rais Magufuli akisisitiza juu ya maagizo ya Waziri Mkuu, aliwataka viongozi wa mikoa na wilaya husika kufanya hivyo sasa na kueleza kwa nini wanaudanganya Mwenge ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

“Waziri Mkuu, nataka yale maelezo ya kina watoe sasa, kwa nini wanadanganya Mwenge, kwa nini wanamdanganya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye ni kiini na mwanzilishi halali wa Mwenge huu,” alisema Rais Magufuli.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post