RAIA WA BURUNDI WALALAMIKIWA KUIBA WAKE ZA WATU ITUMBIKO - KAKONKO

Wananchi  wa Kijiji cha Itumbiko, wilayani Kakonko mkoani Kigoma wamewalalamikia raia wa nchi ya Burundi kuingia kijijini hapo bila vibali na kuwa kero kwa wananchi hao ikiwa ni pamoja na kuwaibia wake zao.

Kero hiyo waliitoa jana kijijini hapo, wakati Mkuu wa Wilaya hiyo,Kanali Hosea Ndagala alipokuwa akisikiliza kero za wananchi , ambapo walimuomba mkuu kumuonya Mwenyekiti wa kijiji hicho kuacha tabia ya kuwaingiza wageni hususani Warundi na kusababisha kero dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwachukulia wake zao na kutoa lugha za vitisho wakati uongozi wa kijiji upo unawaona na taarifa wanapewa lakini hakuna hatua yoyote inayochukuliwa.

Mmoja wa wanakijiji hao, Abel Luhanga  alimuomba Mkuu wa wilaya kuwaondoa Warundi hao ili waweze kuishi kwa amani na kunusuru ndoa zao kutokana na ubabe wanaoutumia kuingia katika vilabu vya pombe na kuwatishia hali inayohatarisha maisha yao na usalama wao. 

"Sisi wananchi wa Itumbiko kero kubwa kijijini, ni ya Warundi kwenye kijiji chetu ambao wanakuja kwa ajili ya kufanya kazi mashambani na wengine wanaonekana kwenye viLabu vya pombe nyakati za jioni, na imefikia hata kutuchukulia wake zetu na kututishia maisha, pale tunapotoa taarifa kwa uongozi wa kijiji na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa',alieleza


Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji cha Itumbiko Benjamini Kahwahwa alipotakiwa kutoa maelezo juu ya kero hiyo ,hakuwa majibu mbali ya kukiri uwepo wa watu hao na kuahidi kuchukua hatua ya kuwaondoa wageni wote kutoka nchi jirani ya Burundi wasiokuwa na vibali. 

Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Kakonko, Juma Maganga aliwaasa wananchi kuheshimu sheria za nchi ,kutokuwaficha wageni ambao baadae wanageuka kuwa majambazi na kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani katika maeneo yao.

Hata hivyo,Mkuu wa wilaya hiyo, Kanali Hosea Ndagala, aliwaomba wananchi kutoa taarifa mapema za wageni wanaoingia kwenye maeneo yao ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka,ikiwa ni pamoja na kukemea tabia ya wananchi ambao wanawaficha Warundi majumbani au mashambani wafute sheria na taratibu zilizopo kama wanataka huduma yao ya kufanya kazi.
 
Aidha kuwaonya viongozi wa kijiji kutumia nyumba kumi za kiusalama kuimarisha ulinzi ikiwa ni pamoja na kuwabaini wageni wote wanaoingia kwenye maeneo yao bila kibali. 

Mkuu huyo wa wilaya alimwagiza Ofisa Uhamiaji wa Wilaya Christopher Mlemeta kufanya msako wa wahamiaji wote walioingia wilayani kutoka nchi jirani na kufanya kazi za kilimo na kijamii bila kibali.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog 
Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akisikiliza kero za wananchi wa kijiji cha Itumbiko - Picha zote na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527