HALOTEL KUWAZAWADIA WATEJA WAKE MAADHIMISHO YA MIAKA 3


Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Halotel Mhina Semwenda,(kushoto) akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa uzinduzi wa mpango wa kutoa ya zawadi kwa wateja wake ambao watatoa mawazo katika kusaidia uboreshaji wa huduma kwa wateja uliopewa jina la Longa Tusonge. Kulia ni Msaidizi wa Mkuu wa kitengo cha Huduma kwa wateja Anthony Thobias.
Msaidizi wa kitengo cha Huduma kwa wateja Anthony Thobias ( kushoto) akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa uzinduzi wa mpango wa kutoa ya zawadi kwa wateja wake ambao watatoa mawazo katika kusaidia uboreshaji wa huduma kwa wateja uliopewa jina la “Longa Tusonge”. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Halotel Mhina Semwenda.

Ikiwa katika shamrashamra ya kuadhimisha miaka 3 ya utoaji wa huduma kwa watanzania, Kampuni ya mawasiliano ya simu ya Halotel, kwa mara ya kwanza imetangaza mpango wa kutoa huduma ya zawadi kwa wateja wake ambao watatoa mawazo katika kusaidia uboreshaji wa huduma kwa wateja.

Mpango huo uliopewa jina la “LONGA TUSONGE” pamoja na faida zingine una lengo la kuwashirikisha wateja wote pamoja na wafanyakazi wa Halotel katika kufanya maboresho ya utoaji huduma mbalimbali kupitia mawazo yao wakati huu ambapo kampuni hiyo inapoadhimisha miaka mitatu ya utoaji huduma zake za Mawasiliano hapa nchini.

Akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Kampuni hiyo, Mhina Semwenda, amesema kuwa, mkakati huo ni sehemu ya kuthamini mchango mkubwa wanaoutoa wateja wake tangu kuanza kutolewa kwa huduma kupitia mtandao huo hapa nchini .

Amesema tangu kuingia kwa huduma za Mtandao huo wa Halotel, wamekuwa wakipata matokeo mazuri ya wateja wake wanaondeelea kutumia huduma zake mbalimbali hadi wakati huu ambapo wanakuja na mpango huo mpya wa “LONGA TUISONGE”

Amesema kupitia mpango huo wa mwaka mmoja, wateja wa mtandao huo watapewa nafasi ya kutoa mawazo yao mbalimbali ya kuboresha huduma za Halotel ambayo baadae yatachujwa na kwa yale yatakayokidhi matakwa yatapitishwa na kuwa huduma rasmi ndani ya mtandao huo.

“Hii fursa kubwa kwa wateja wetu walioko nchi nzima katika kutambua na kuthamini mchango wao mkubwa ambao wamekuwa wakituunga mkono tangu tuanze kutoa huduma za mawasiliano hapa nchini. Lengo letu kubwa ni kuhakikisha wanaendelea kupata huduma bora za mawasiliano zinazotokana na mahitaji yao katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi kupitia Mtandao wa Halotel.” Alisema Semwenda.

Amesema huo ‘LONGA TUSONGE” ni mpango Shirikishi unaolenga kupokea mawazo mbalimbali ya wateja wake wote ili kujua kitu gani wangependa kiboreshwe au kiongozwe katika huduma zinazotolewa hatua ambayo pamoja na mambo mengine itawasaidia kuendelea kunufahika na huduma za mtandao huo.

Aidha mkuu huyo wa mawasiliano amesema zawadi hizo zitatolewa kwa wateja watakaotoa mawazo bora kupitia mitandao ya kijamii ya kampuni hiyo, namba ya huduma kwa wateja, maduka ya Halotel yaliyopo nchi nzima, pamoja na barua pepe (callcentre@halotel.co.tz). Zawadi zitakazotolewa kwa washindi wenye mawazo bora ni pamoja na Simu aina ya smatiphone, Muda wa maongezi, 4G router, na fedha Taslimu.

“Zawadi hizi ni moja ya mikakati ya kutoa motisha kwa wateja wetu na watanzania kwa ujumla ikiwa ni moja ya shukrani yetu kwao katika shamrashamra za kuadhimisha miaka 3 ya kutoa huduma hivyo Halotel ni mtandao wao na wanao uhuru wa kushiriki katika kutoa maoni kuhusu namna ambavyo sisi kama kampuni tunaweza kuboresha huduma. Aliongeza Semwenda.

“Tunapenda kuwaalika wateja wetu wote walioko nchi nzima kushiriki kikamilifu katika mpango huu, na sisi kama kampuni tuko tayari kuwasilikiza, kuyapokea na kuyafanyia kazi maoni yao ambayo yatazidi kuwa chachu ya kutoa huduma bora”. Alisisitiza Semwenda

Aidha aliongeza kuwa mtandao wa Halotel ambao huduma zake zinapatikana maeneo mengi nchini itandelea kujikita zaidi na zaidi katika kutoa huduma bora kwa wateja wake wote ikiwa ndiyo sababu kuu ya kuanzishwa kwake hapa nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527